1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi dhidi ya washirika wa Saddam Hussein yasikilizwa

Josephat Charo21 Agosti 2007

Washirika 15 wa kiongozi wa zamani wa Irak, Saddam Hussein, wamefikishwa mahakamani hii leo mjini Baghdad kujibu mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu kwa kuhusika na mauaji ya halaiki wakati wa ukandamizaji wa mapinduzi ya Washia ya mwaka wa 1991.

https://p.dw.com/p/CB1s
Ali Hassan al Majid ´Chemical Ali´
Ali Hassan al Majid ´Chemical Ali´Picha: picture-alliance/dpa

Washukiwa watatu akiwemo binamu yake Saddam Hussein, Ali Hassan al Majid, kwa jina maarufu Chemical Ali, tayari walihukiwa kifo katika kesi nyengine ya awali kwa mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu. Majid alikuwa wa kwanza kuingia mahakama ya mjini Baghdad akiwa amevaa vazi la rangi ya malai, kitambaa cheupe kichwani na fimbo yake mkononi.

Wakati jaji Mohammed al Oreibi al Khalifah alipomuuliza ajitambulishe, al Majid alijibu na hapa namnukulu, ´Mimi ndiye mpiganaji Ali Hassan al Majid,´ mwisho wa kumnukulu. Muongozaji mashtaka katika matamshi yake ya kwanza amemshitaki Majid kwa mauji ya umwagaji damu wakati jeshi la Saddam Hussein kusini mwa Irak lilipokuwa likiwaua maelfu ya Washia wakati walipofanya mapinduzi baada ya kumalizika vita vya Ghuba mnamo mwaka wa 1991.

Helikopta ziliishambulia miji kwa mabomu na nyumba za raia. Wafungwa waliokamatwa waliuwawa, amesema muongozaji mashtaka ambaye jina lake halikutajwa kwa sababu za usalama. Amesema Majid alikuwa akienda katika vituo vilivyotumiwa kuwazuilia watu, kuwafunga mikono wafungwa na kuwaua kwa kuwapiga risasi kutumia bunduki yake. Halafu maiti zilizikwa kwenye makaburi ya halaiki, ambayo mengi yamegunduliwa tangu vita vya Irak vilipomalizika. Kuna makaburi mengine yanayoweza kupatikana iwapo yataendelea kutafutwa.

Waongozaji mashtaka wanadai Washia kufikia laki moja waliuwawa wakati wafuasi wa Saddam Hussein walipoyazima mapinduzi ya Intifada ya mwaka wa 1991, yaliyoanzishwa na wanajeshi waliokimbia jeshi la Irak baada ya kushindwa katika vita nchini Kuwait na katika mapinduzi ya Wairaki.

Mauaji ya halaiki yalitokea katika miji mitakatifu ya Washia ya Najaf na Karbala na katika maeneo ya Hilla na Basra baada ya jeshi la muungano lililoongozwa na Marekani kuamua kusitisha harakati yake nchini Irak.

Saddam alipopoteza majimbo ya kusini mwa Irak aliamuru vifaru viondoke Kuwait na kuishambulia miji ya Basra na Maysa. Kiongozi huyo alifanya uamuzi wa haraka na kumuaru Majid aharibu kila kitu na kuua mtu yeyote aliyejaribu kupingana na vikosi vya Irak.

Shahidi wa kwanza, mwanajeshi wa zamani, Raybath Jabbar Risan, mwenye umri wa miaka 65, amesema kijiji chake kilikaliwa na wanajeshi wa Saddam. Alifanya kazi katika jeshi la Irak kwa miaka 30 na hakufiri jeshi hilo lingekishambulia kijiji chake mkoani Basra kwa makombora na risasi. Amesema binamu yake aliuwawa na mpwa wake kujeruhiwa vibaya. Nyumba ya kakake ilichomwa moto lakini yeye akakimbia pamoja na familia yake.

Mmoja wa washtakiwa Sabbawi al Ibrahim, aliyekuwa mkurugenzi wa ujasusi katika utawala wa Saddam, ameiambia mahakama kwamba maafisa wa ujasusi wa Iran walichochea mapinduzi ili kuua na kupora.

Amesema hajawahi kukaa mjini Amara kwa angalau dakika 30 katika maisha yake yote lakini anashangaa kwa nini leo anashtakiwa kwa mauaji ya watu wa Amara. Ameongeza kusema Iran ilishindwa kutimiza ilichokitaka mnamo mwaka wa 1988 ndio maana ikautumia wakati Irak ilipokuwa dhaifu na maafisa wake wa ujasusi wakaliliingilia eneo la kusini mwa Irak.

Sultan Hashim al Tai, waziri wa zamni wa ulinzi, na Hussein Rashid al Tikriti, naibu kamanda wa jeshi, pia walihukumiwa kifo katika kesi ya mauaji ya halaiki na ni miongoni mwa washtakiwa. Jopo la mahakama lenye wanachama tisa linachunguza hukumu ya kifo dhidi ya Majid, Tai na Tikriti na litatoa uamuzi wake hivi karibuni.

Ikiwa jopo hilo litaidhinisha hukumu hiyo, washukiwa hao watatu watangongwa katika kipindi cha siku 30 zijazo kwa mujibu wa sheria ya Irak. Kwa hiyo mashtaka yanawakabili hivi sasa yatafutwa.