1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya Demjanjuk yafunguliwa mjini Munich

Oumilkher Hamidou30 Novemba 2009

Mtuhumiwa wa miaka 89- Demjanjuk akabiliwa na kifungo cha maisha akikutikana na hatia ya kuwauwa wayahudi huko Sobibor

https://p.dw.com/p/Kl6j
Mtuhumiwa John Iwan DemjanjukPicha: AP

Kesi ya John Iwan Demjanjuk,mwenye umri wa miaka 89,anaetuhumiwa kuchangia katika kuteketezwa wahayudi 27 900 katika kambi ya maangamizi ya wanazi huko Sobibor,imefunguliwa leo,baada ya kucheleweshwa kutokana na msongomano wa watu.

Mtuhumiwa,wa mwanzo katika orodha ya wahalifu wa vita ambao bado wahai,kufuatana na orodha iliyoandaliwa na kituo cha Simon Wiesenthal,ameletwa katika ukumbi wa mahakama akiwa katika kiti cha wagonjwa kutokana na hali yake mbaya ya afya.

Bwana huyo asiyekua na uraia wa nchi yoyote,mwenye asili ya Ukraine,anakabiliwa na kifungo cha maisha pindi mahakama ya mjini Munich ikiamua kwamba yeye ndie aliyekua mlinzi wa kambi ya maangamizi ya Sobibor nchini Poland, kwa muda wa miezi sita mnamo mwaka 1943.

Mwanasheria mkuu,Babara STOCKINGER anasema:

"Mtuhumiwa Demjanjuk alikua mlinzi wa kambi ya Sobibor na amehusika na kuangamizwa wayahudi.Tangu mwanzo alikua akihakikisha gari linalowasafirisha wayahudi linapofika, anafanya kila la kufanya kuona wanapelekwa katika chumba cha gesi ."

Katika kipindi hicho wayahudi 27 elfu wakiwemo pia wayahudi wa kutoka Uholanzi waliuliwa kwa gesi.

Demjanjuk anakanusha akisema hajawahi kuwa mlinzi wa kambi ya maangamizi ya Sobibor.

Akivalia kikofia cha baseball na koti jeusi,amefunikwa blangeti la rangi ya buluu isiyokoza kuanzia magotini mpaka chini.Wakati wote kesi ilipokua ikiendelea alikua akifumba macho aliyoyafunika kwa miwani .Amekua akilindwa na walinzi wawili na kushughulikiwa na wauguzi wawili.

Kesi ya mtuhumiwa huyo inayotajikana kua mojawapo ya kesi kubwa kabisa za uhalifu wa vita uliofanyika wakati wa utawala wa wanazi,imekawia kuanza kutokana na mikururo ya watu waliokua wakiingia katika ukumbi wa mahakama.

Ukumbi huo wa mahakama haupokei zaidi ya watu 150,katika wakati ambapo walionusurika na mauwaji ya halaiki ya Holocaust,au jamaa zao na waandishi habari wa kutoka kila pembe ya dunia wamemiminika kusikiliza kesi hiyo.

Prozess John Demjanjuk Montag 30.11.2009 Landgericht München
Korti ya mjini Munich inakoendelea kesi dhidi ya DemjanjukPicha: picture-alliance / dpa

Roben Cohen,mholanzi mwenye umri wa miaka 83 ni miongoni mwa waliotuma mashtaka dhidi ya Demjanjuk.Yeye amesalimika katika kambi za maangamizi,ikiwemo pia kambi ya Auschwitz,lakini familia yake imeteketezwa katika kambi ya Sobibor.

"Kama Demjanjuk alikuwepo huko,basi ameuwa zaidi ya watu mia moja kwa siku.Ni uhalifu uliokithiri" amewaambia waandishi habari huku akionyesha chapa aliyopigwa,wakati alipokua akishikiliwa katika kambi ya maangamizi.

""Sijali adhabu atakayopewa,nnachotaka ni haki." amesema Max Flam,mholanzi mwenye umri wa miaka 43,anaemuakilisha mamaake mwenye umri wa miaka 90 ambae ni miongoni mwa wanaoshitaki.Afya ya bibi huyo mzee haijamruhusu kuondoka Amsterdam.

Hii ni mara ya kwanza kwa mgeni kuhukumiwa nchini Ujerumani kwa uhalifu uliofanywa wakati wa utawala wa wanazi.

Mwandishi:Hamidou,Ommulkheir/ AFP

Mhariri:Abdul-Rahman