1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya Ghailani yaanza, Marekani.

Halima Nyanza30 Septemba 2010

Kesi ya mfungwa aliyekuwa akishikiliwa katika gereza la Guantanamo imeanza kusikilizwa katika mahakama ya mjini New York, Marekani, hii ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika kesi ya aina hiyo.

https://p.dw.com/p/PQXu
Mtanzania Ahmed Khalfan Ghailani, anayetuhumiwa kusaidia mashambulio ya kigaidi katika ubalozi wa Marekani, Kenya na tanzania mwaka 1998.Picha: AP

Mtanzania, Ahmed Khalfan Ghailani ambaye anatuhumiwa kuhusika na mauaji ya watu 224 katika shambulio la mabomu lililotokea mwaka 1998 dhidi ya ubalozi wa Marekani nchini Tanzania na Kenya, alionekana akitabasamu na kutaniana na mawakili wake wakati zoezi la kuwachagua wajumbe wa baraza la mahakama lilipokuwa likiendelea katika chumba cha mahakama mjini New York.

Bild des ersten Guantanamo-Häftlings vor einem US Zivilgericht: Ahmed Ghailani
Ahmed Ghailani,(Kushoto) akiwa katika mahakamani.Picha: AP

Ingawa ulinzi ulikuwa mkali ndani ya mahakama hiyo ambayo iko jirani na eneo lilipokuwa kituo cha biashara cha kimataifa kilichoteketezwa wakati wa shambulio la kigaidi la Septemba 11, maeneo kuzunguuka eneo hilo ilikuwa katika hali ya kawaida, huku watalii, wafanyakazi na wakaazi wa eneo hilo wakiendelea na shughuli zao.

Jana Jaji Lewis Kaplan alichuja jopo la wajumbe hao, ambao hawatajulikana muda wote wa uendeshaji kesi hiyo.

Amefafanua kuwa yeye na wanasheria wa pande zote mbili walikubaliana kupunguza jopo hilo, kutoka mamia ya watu hadi kufikia watu 12, ikiwemo wale wa akiba, ifikapo Jumatatu.

Na katika kuonesha kuwa kesi hiyo ni nyeti, Jaji Kaplan  alisisitizia kuhakikishia majaji wa baraza la mahakama kwamba majina yao, sehemu wanazofanyia kazi na makaazi yao hayatawekwa hadharani.

Aidha amesisitizia pia umuhimu wa wajumbe hao wa baraza la mahakama kuepukana na kujadiliana na marafiki zao ama waandishi wa habari kuhusiana na kesi hiyo nzito. 

Hoja za ufunguzi wa kesi hiyo zinatarajiwa kuanza rasmi Jumatatu ijayo, katika kesi hiyo ambayo inatarajiwa kusikilizwa kwa miezi kadhaa na kuwa jaribio la juhudi za Rais Obama kulifunga gereza hilo la Guantanamo  na hatimaye watuhumiwa hao wa ugaidi kuingizwa katika mfumo wa sheria wa kiraia. 

Mwaka jana, Ghailan alikanusha kusaidia mipango ya shambulio hilo la mabomu katika ubalozi wa Marekani Dar es Salaam, Tanzania, huku bomu jingine likilipuka katika muda huohuo kwenye ubalozi wa Nairobi Kenya.

Anadaiwa pia kuwa msaidizi wa karibu wa Osama bin Laden.

Osama bin Laden
Osama bin Laden.Picha: AP

Wanasheria wake walijaribu kuizuia kesi hiyo, wakihoji kuwa  haki za kisheria za mteja wao zimekuwa zikikandamizwa kutokana na kuteswa katika gereza la siri la shirika la Ujasusi la marekani CIA, na pia kuwekwa kizuizini kwa miaka mitano, ikiwemo katika gereza la Guantanamo, kabla ya kesi yake kusikilizwa mahakamani.

Anakabiliwa na kifungo cha maisha, iwapo atatiwa hatiani.

Kesi hiyo ni mtihani kwa Rais wa nchi hiyo Barack Obama kwa ahadi yake ya kumaliza mateso na ukiukaji wa haki katika vita dhidi ya ugaidi. Kwa mara ya kwanza kesi hiyo ilisikilizwa jana Jumatano.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp)

Mhariri: Josephat Charo