1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya Hayati Oury Jalloh itarejewa upya

Miraji Othman8 Januari 2010

Mahakama kuu ya Ujerumani yataka kesi juu ya marehemu Jalloh irejewe upya

https://p.dw.com/p/LOZX
Mamadou Saliou Diallo, ndugu wa marehemu Oury Jalloh, akizungumza pembezoni mwa mahakama ya Dessau-Rosslau hapo Disemba mwaka 2008 juu ya kesi ya marehemu ndugu yake.Picha: picture-alliance/ dpa

Ile kesi iliohusiana na inavosemakana kujiuwa mwenyewe mwombaji ukimbizi, raia wa Sierra Leone, Oury Jalloh, alipokuwa katika ulinzi wa polisi hapa Ujerumani miaka mitano iliopita, sasa itarejewa tena. Jana, mahakama kuu ya Ujerumani mjini Karlsruhe ilitupilia mbali hukumu ya kumuachia huru afisa wa polisi aliyekuwa akimchunga Muafrika huyo na ambayo ilitolewa na mahakama ya mkoa huko Dessau. Jumuiya za kupigania haki za binadamu na zile za Waafrika zimeipokea kwa uzuri hukumu hiyo ya mahakama kuu .

Kwa mujibu wa mahakama kuu ya Karlsruhe ni kwamba hukumu ilitolewa na mahakama ya mkoa huko Dessau hapo Disemba 28 inaonesha ilikuwa na walakini katika mlolongo wa ushahidi. Sasa miaka mitano baada ya kufa Muafrika huyo wa kutokea Sierra Leone, ambaye aliomba hifadhi ya ukimbizi hapa Ujerumani, itabidi kesi hiyo dhidi ya afisa wa polisi irejewe upya. Mahakama kuu ilitupilia mbali hukumu ya kutomuona na hatia afisa huyo wa polisi aliyekuwa kazini wakati wa kifo cha Oury Jalloh.

Oury Jalloh aliungua moto hapo Hanuari 7 mwaka 2005 wakati akiwa amefungwa mikono yake ndani ya chumba cha mahabusu. Kwa mujibu wa polisi ni kwamba yeye mwenyewe aliuasha moto huo. Kwa mujibu wa mahakama kuu ni kwamba hali ya karibu iliokuweko wakati huo haitoi mwangaza ulio wazi vipi muombaji huyo wa hifadhi ya ukimbizi hapa Ujerumani aliweza mwenyewe kuuwasha moto huo.

Kufunguliwa upya kesi hiyo ni muhimu kwa vile kutarejesha imani ya wahamiaji ambao ni wenye kuguswa sana linapokuja suala la watu kupewa haki zao kupitia mahakama. Kwa mujibu wa afisa wa serekali anayeshughulikia masuala ya kuwachanganyisha wahamiaji katika jamii ya Ujerumani kwenye mkoa wa Sachsen-Anhalt, Susi Möbbeck, ni kwamba nanma uchunguzi wa kesi hiyo ulivofanywa umeifanya imani ya wahamiaji hao kuingia mashakani. Naye rais wa kanisa katika mkoa wa Sachsen Anhalt, Joachim Liebig, alisisitiza kwamba kama afisa huyo wa polisi alikuwa mkosa au si mkosa mwishonwe itajulikana tu pale kisa hicho cha kutisha kitapowekwa wazi bila ya ati ati yeyote.

Marafiki na jamaa wa Oury Jalloh walisema hukumu hiyo ya Karlsruhe ilikuwa ya haki, na makamo wa rais wa Jumuiya ya kimataifa ya kupigania haki za binadamu, Yonas Endrias, alisema angetaka kumkumbatia hakimu aliotoa hukumu hiyo kwa kila sentensi alioisema:

"Tunafurahi kwamba leo ni siku nzuri kwa haki za binadamu katika Ujerumani. Huko Dessau haki haijaonekana kutoka upande wa polisi, wa hakimu na wa mji wa Dessau, lakini leo ni siku ya furaha sana, kwa vile wanaopigania wote wa haki za binadamu watakuwa na furaha, kwa vile leo tunaweza kufurahia hukumu ya haki itakayopelekea kupata mwangaza juu ya hali ya kifo cha Oury Jalloh."

Pia kulitolewa mwito wa kuundwa tume huru ya uchunguzi kuhusu mkasa huo.

Jana watu 250 huko Dessau-Rosslau waliikumbuka siku aliofariki Oury Jalloh. Licha ya kuweko sala ya ukumbusho, akishiriki pia meya wa Dessau, pia asubuhi kuliwekwa mishumaa katika mlango wa ofisi ya polisi ambako Oury Jalloh alikufa. Watu 170 walishiriki katika maandamano yalioandaliwa na vyama mbali mbali vya kuwatetea wakimbizi. Chama cha Kijani pia kimeikaribisha hukumu hiyo, kilisema kwamba kesi ya kwanza huko Dessau-Rosslau tangu mwanzo ilikuwa ni mzaha na ilikuwa haina nia ya kutafuta ukweli.

Katika hati ya mashtaka dhidi ya polisi huyo ilitajwa kwamba iliwezekana kumnusuru Jalloh pindi afisa huyo wa polisi angechukuwa hatua kwa wakati, tena hatua zilizo barabara. Ilitajwa kwamba Polisi walimfunga mikono Jalloh kwa vile alikuwa anawasumbua wasafishaji wa kike na ambao waliomba msaada. Polisi aliyeshtakiwa alimzwia Muafrika huyo kwa vile alikuwa anataka kuchunguza juu ya makaratasi yake ya ukaazi, licha kwamba yeye alikuwa akimjuwa.

Binadamu anaungua akiwa katika ulinzi wa polisi. Kwamba mtu huyo alifungwa mikono yake na ati mwenyewe alilichoma godoro aliilokuwa akilalia ni hadithi inayotia wasiwasi. Kwamba mahakama na wananchi wanataka kujuwa zaidi juu ya mkasa huo ni jambo linaloeleweka. Bila ya kujali vipi mwishowe kesi hii dhidi ya polisi aliyemkamata Oury Jalloh itakavomalizika, kesi za mwanzoni zimedhihirisha kwamba polisi huyo ingembidi afanye zaidi kuyaokoa maisha ya hayati huyo ili kutoa sura kwamba watu wanaoishi hapa Ujerumani wanahisi kwamba polisi wao ni marafiki na wasaidizi pia. Ndio maana watu wengi wameipa hongera hukumu ya jana ya Karlsruhe ambayo imechangia kuleta usalama kwa msingi wa haki.

Mwandishi. Miraji Othman/epd

Mhariri: Aboubakar Liongo