1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya kwanza ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu kunguruma Jumatatu.

Sekione Kitojo23 Januari 2009

Miaka saba tangu kuundwa kwa mahakama ya kimataifa ya kuwahukumu wahalifu wa kivita, ICC, mahakama hiyo itaanza kusikiliza kesi yake ya kwanza siku ya Jumatatu

https://p.dw.com/p/Gf3q

Karibu miaka saba tangu kuundwa, mahakama ya kimataifa ya kuwahukumu wahalifu ICC, itaanza kusikiliza kesi yake ya kwanza siku ya Jumatatu, kesi ambayo inamhusu kiongozi wa waasi wa Congo Thomas Lubanga kwa madai ya kuwatumia watoto kama wanajeshi katika vita nchini humo.

Lubanga anakabiliwa na mashtaka matatu ya uhalifu wa kivita kwa madai ya kuwatumia mamia ya watoto chini ya umri wa miaka 15 katika mapigano katika jimbo la Ituri ya mashariki la jamhuri ya kidemokrasi ya Congo kati ya Septemba 2002 na august 2003.

Kesi hiyo inatarajiwa kuanza kusikilizwa kwa kuanza kusomwa muhtasari wa taarifa , itakayosomwa na mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo Luis Moreno-Okampo, ikifuatiwa na mawakili wa wahanga wa madhara ya wanajeshi wa Lubanga, na baadaye upande wa utetezi.

Shahidi wa kwanza , ambaye ni mwanajeshi wa zamani mtoto,atapanda kizimbani siku ya Jumatano, akifuatiwa na baba yake , kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na na ofisi ya mwendesha mashtaka.

Kutakuwa na mashahidi 30 kwa jumla, ikiwa ni pamoja na wanajeshi watoto binafsi, wanajeshi wa zamani wa kundi hilo la wanamgambo waliohusika katika mapigano katika jimbo la Ituri, na wataalamu katika masuala hayo ambao wataamua kuhusu umri wa watoto hao.

Kesi hii inahusu kutoa ishara kali , kuwa ni vibaya kiasi gani kuwaandikisha watoto kuwa wanajeshi na kuwafanya wawe wauaji , amesema mwendesha mashtaka huyo wakati akihojiwa na shirika la habari la AFP ofisini kwake.

Amesema kuwa kesi hiyo itatoa picha mbaya ya kile kinacholazimisha kuwa mwanajeshi mtoto. Kama watu wazima ameongeza tuna wajibu wa kuwaelimisha watoto wetu. Na hapa watoto wanafundishwa kuua, wanafundishwa utekaji nyara , uporaji, na ubakaji.

Lubanga mwenye umri wa miaka 48, kutoka kabila la Hema alikuwa mfanyabiashara wa kuuza vyakula kabla ya kuwa mbabe ya kivita anayeogopewa akiongoza moja kati ya makundi sita yenye silaha yanayowania udhibiti katika eneo la mashariki ya jamhuri ya kidemokrasi ya Congo lenye utajiri mkubwa wa madini la Ituri.

Eneo hilo limekuwa limekumbwa na miaka kadha ya mizozo kati ya watu wa kabila la Hema na Lendu ambao wanafanya asilimia 40 ya watu wa jimbo hilo la kaskazini mashariki ya Congo.

Lubanga haraka alijitokeza kuwa kiongozi mwenye haiba na mlinzi wa jamii yake akiongoza kundi la Union of Congolese Patriots UPC, ama umoja wa wazalendo wa Congo, ambalo lilikuwa na tawi lake la kijeshi la FPLC lilikamata maeneo kadha muhimu ya machombo ya madini katika mkoa wa Ituri.

Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka, Lubanga , alizishawishi familia za Wahema kuwatoa watoto wao kwenda kujiunga na UPC na kuwaweka katika maeneo ya mapambano kati ya Septemba 2002 na August 2003.

Kundi hilo la wanamgambo linatuhumiwa kufanya mauaji kadha ya raia wa kabila la Lendu kati ya mwaka 2002 na 2003, hususan katika ngome yake kuu katika mji wa Bunia mji mkuu wa jimbo la Ituri.

Lubanga alikimbia kutoka Bunia baada ya jeshi la umoja wa Ulaya kuwekwa katika eneo hilo Juni 2003 ili kusitisha umwagaji damu.

Aliibukia mjini Kinshasa , 2004 ambako alikuwa akiishi hotelini wakati akisubiri kupandishwa wadhifa katika cheo cha jenerali, ahadi iliyotolewa na serikali kwa wakuu wote wa makundi ya wanamgambo ambao wamekubali kuweka silaha chini.

Lakini kurejea tena kwa machafuko katika jimbo la Ituri na kuuwawa kwa wanajeshi tisa wa kulinda amani wa umoja wa mataifa Februari , 2005 kulisabibisha kukamatwa kwa Lubanga na maafisa wa Congo mwezi uliofuatia.


►◄