1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya Mauwaji ya halaiki ya Rwanda Paris

4 Februari 2014

Miaka 20 baada ya mauwaji ya halaiki ya Rwanda,Ufaransa iliyokuwa ikituhumiwa kuunga mkono waliofanya mauwaji hayo,inamhukumu kwa mara ya kwanza afisa wa zamani wa Rwanda kwa mchango wake katika mauwaji hayo.

https://p.dw.com/p/1B2Lz
Madaftari ya mashtaka dhidi ya Pascal Simbikangwa katika ukumbi wa korti mjini ParisPicha: Martin Bureau/AFP/Getty Images

Baada ya kukamatwa mnamo mwaka 2008 katika kisiwa cha Mayotte katika bahari ya Hindi alikokuwa akiishi kwa jina bandia,Pascal Simbikangwa anafikishwa mahakamani kuambatana na kanuni za Ufaransa zinazoipa "uwezo wa kisheria usiokuwa na mpaka" na kuiruhusu nchi hiyo kuwaandama watu wanaosakwa kwa makosa ya uhalifu dhidi ya ubinaadam waliyoyafanya nchi za nje.

Vyombo vya sheria vya Ufaransa vinapinga,kama kawaida,kumrejesha Rwanda kepteni huyo wa zamani wa kabila la hutu.Akikutikana na hatia atafungwa kifungo cha maisha.

Akiwa na umri wa miaka 54,Pascal Simbikangwa anafikishwa mahakamani kuanzia leo hii kwa makosa ya kula njama katika mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya ubinaadam..Anatuhumiwa kuchochea,kuandaa na kusaidia na hasa katika kuweka vizuwizi na kuwapatia silaha wanamgambo waliowauwa watu wasiopungua laki nane kwa muda wa siku 100 kati ya mwezi wa april na Julai mwaka 1994.

Kepteni huyo wa zamani aliyejiunga katika kikosi cha askari kanzu baada ya ajali iliyopelekea kupoteza nguvu za miguu yake mwaka 1986,anakanusha tuhuma zote dhiti yake.

Keshi dhidi ya kula njama

Kesi hiyo ya aina yake imepangwa kudumu hadi wiki nane.Siku ya leo itatumika kumsomea mashtaka dhidi yake na kuanza kuulizwa masuala kuhusu wasifu wake.

Prozess gegen Pascal Simbikangwa in Paris 04.02.2013
Ukumbi wa korti inakosikilizwa kesi ya kula njama katika mauwaji ya halaiki dhidi ya kepteni wa zamani wa Rwanda Pascal SimbikangwaPicha: Martin Bureau/AFP/Getty Images

Simbikangwa anakiri alikuwa karibu sana na kundi la "Akazu" au nyumba ndogo ambalo viongozi wake kadhaa wamekutikana na hatia ya kuhusika na mauwaji ya halaiki.Lakini anakanusha moja kwa moja kuhusika binafsi na mauwaji ya halaiki na mawakili wake Alexandra Bourgeot na Fabrice Epstein wanakosoa kile wanachokiita " madaftari finyu" ambamo tuhuma pekee zinatokana na ushahidi.

Mahakama ya Ufaransa imeachilia mbali tuhuma za kuhusika na mauwaji ya halaiki badala yake anashitakiwa kuhusika na kula njama katika mauwaji hayo ya halaiki.

Mashahidi zaidi ya 30 watasikilizwa

Mashahaidi zaidi ya 30 wa kinyarwanda watasikilizwa, ikiwa ni pamoja na ushahidi kupitia njia ya video wa wale wafungwa waliohukumiwa na mahakama ya kimataifa ya kimataifa ya mjini Arusha au na mahakama ya Rwanda.

Ruanda Völkermord 1994 Hutu Tutsis Gedenkstätte Nyamata
Makumbusho ya Nyamata yanakokutikana mabufuu na mifupa ya wahanga wa mauwaji ya halaiki ya mwaka 1994 nchini RwandaPicha: AP

Mawakili wa mshitakiwa wanakosoa kile wanachokiita kesi ya kisiasa na kidiplomasia katika wakati ambapo serikali za Kigali na Paris iliyokuwa ikituhumiwa na viongozi wa serikali ya Rwanda kuwaunga mkono waliofanya mauwaji ya halaiki,zimeanza kujongeleana baada ya miaka mitatu ya mtengano wa kidiplomasia kati ya mwaka 2006-2009.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman