1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya Mubarak kuendelea tena leo

Josephat Nyiro Charo28 Desemba 2011

Kesi ya rais wa zamani wa Misri ,Hosni Mubarak inaanza tena leo (28.12.2011) mjini Cairo, baada ya kipindi cha miezi mitatu kilichoshuhudia machafuko ya umwagaji damu na vyama vya Kiislamu vikishinda uchaguzi wa bunge.

https://p.dw.com/p/13aVr
Hosni Mubarak akiwa mahakamani mwezi Septemba 2011.
Hosni Mubarak akiwa mahakamani mwezi Septemba 2011.Picha: picture-alliance/dpa

Mubarak mwenye umri wa miaka 83 anashtakiwa kwa kuamuru mauaji ya watu takriban 850 wakati wa maandamano ya mapinduzi ambayo hatimaye yalimuondoa madarakani. Anakabiliwa na hukumu ya kifo iwapo atatiwa hatiani kwa kuhusika na mauaji hayo. Kesi ya leo inasikilizwa katika chuo cha mafunzo cha jeshi la polisi nje kidogo ya mji mkuu, Cairo.

Kiongozi huyo wa zamani ambaye anazuiliwa katika hospitali ya kijeshi mjini Cairo, pia anakabiliwa na mashtaka ya rushwa pamoja na wanawe wawili wa kiume Alaa na Gamal. Waziri wa zamani wa mambo ya ndani wa Misri, Habib al-Adly, na maafisa sita wa usalama pia wanakabiliwa na mashtaka kwa jukumu lao katika kuyazima maandamano. Washtakiwa wote wamekanusha mashtaka yote dhidi yao.

Wizara ya mambo ya ndani imesema zaidi ya maafisa 5,000 wa polisi watapelekwa kulinda usalama wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo. Licha ya ulinzi mkali wakati wa kusikilizwa kwa kesi ya Mubarak hapo awali, makabiliano makali yalizuka kati ya wafuasi na wapinzani wa kiongozi huyo nje ya mahakama, ambapo watu kadhaa walijeruhiwa na wengine kutiwa mbaroni.

Kesi ya Mubarak ilionyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni iliposikilizwa kwa mara ya kwanza Agosti 3, lakini jaji aji aliyekuwa akiiskiliza, Ahmed Refaat, aliamuru kesi hiyo isionyeshwe tena kwenye televisheni.

Waziri katika serikali ya Mubarak, Anas al-Fiq, akisikiliza mashitaka yake mahakamani.
Waziri katika serikali ya Mubarak, Anas al-Fiq, akisikiliza mashitaka yake mahakamani.Picha: picture alliance/dpa

Kesi hiyo ilisitishwa wakati mawakili wa Mubarak walipowasilisha ombi kutaka jaji Refaat aondolewe kwa madai alikuwa akiwapendelea walalamishi. Ombi hilo lilikataliwa tarehe 7 mwezi huu.

Mubarak ni kiongozi wa kwanza kung'olewa madarakani wakati wa maandamano ya msimu wa mapukutiko katika mataifa ya kiarabu kufikishwa mahakani. Licha ya hamasa kubwa ya vyombo vya habari wakati wa kuanza kesi yake, hatima yake imegubikwa na makabiliano makali kati ya jeshi na waandamanaji wanaoupinga utawala wa kijeshi wa Misri uliotwaa madaraka wakati rais Mubarak alipojiuzulu.

Macho pia yalielekezwa zaidi kwenye uchaguzi wa bunge baada ya mapinduzi, ulioanza Novemba 28, ambapo vyama vya Kiislamu vimeongoza katika matokeo.

Inatarajiwa kwamba kuanza tena kwa kesi ya rais huyo wa zamani wa Misri, utakuwa utaratibu tu, huku kukifanyika majadiliano mafupi kuhusu madai dhidi ya Mubarak. Lakini mawakili wanaomuunga mkono kiongozi huyo wa zamani wana matumaini ya kulisafisha jina lake. Yussri Abdel Razek, anayeongoza kamati ya utetezi, inayowajumuisha pia mawakili kutoka Kuwait, alisema hapo jana kwamba amepata nyaraka mpya zitakazothibitisha Mubarak hana hatia.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/DPAE
Mhariri: Saumu Yusuf