1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Khaled Meshaal kuhudhuria sherehe ya Hamas

8 Desemba 2012

Baada ya kukaribishwa kishujaa akirejea kutoka miongo kadhaa ya kuishi uhamishoni, kiongozi wa Hamas Khaled Meshaal atashereheka kuanzishwa kwa chama cha Hamas leo (08.12.2012), na "ushindi" dhidi ya Israel.

https://p.dw.com/p/16yP4
Khaled Meshaal akiwa na waziri mkuu wa Gaza, Ismail Haniya.
Khaled Meshaal akiwa na waziri mkuu wa Gaza, Ismail Haniya.Picha: Reuters

Wapalestina wasiyopungua 200,000 wanatarajiwa kuhudhuria sherehe hiyo, ambayo inaweza kutumiwa na Meshaal kuendeleza hadhi inayozidi kukua ya chama cha Hamas katika ulimwengu wa Kiarabu, na kushinikiza mapatano na mahasimu wao wa kisiasa, chama kisichoegemea nadharia za kidini cha Fatah. Meshaal mwenye umri wa miaka 56 yuko katika ziara yake ya kwanza kabisa katika ukanda wa Gaza na alishindwa kujizuwia kutokwa machozi kutokana na mapokezi aliyoyapata siku ya Ijumaa kutoka kwa makundi yaliyokuwa yanapeperusha bendera, wakati akizuru eneo hilo dogo linalokaliwa na wapalestina milioni 1.7.

Khaled Meshaal akiwa na Ismail Haniya wakiwapungia watu waliokuja kumlaki kiongozi huyo wa juu wa Hamas.
Khaled Meshaal akiwa na Ismail Haniya wakiwapungia watu waliokuja kumlaki kiongozi huyo wa juu wa Hamas.Picha: Reuters

Israel yaipuuzia ziara yake

Ziara yake imekuja wiki mbili tu baada ya vita vya siku nane Hamas ilivyopigana na Israel ambapo wapalestina 170 waliuawa na Waisrael sita, na kumalizika kwa makubaliano yaliyoratibiwa na Misri. Hamas inadai ilishinda vita hivi lakini Israel inapingana na madai hayo. Israel inasema si tu ilimuua kamanda wa kijeshi wa Hamas, lakini pia ilifanya uharibifu mkubwa katika ghala ya maroketi ya Hamas. Vyombo vya habari vya Israel vimepuuzia ziara hii ya Meshaal mjini Gaza.

Hakuna ubishi kwamba vita hivyo vimeongeza umaarufu wa Hamas katika kanda ya mashariki ya kati, na kuipatia uungwaji mkono na majirani wa Kiarabu, ambao huko nyuma walikuwa wanakichukulia kama chama cha waasi kabla ya maandamano yaliyopelekea kuingia madarakani, kwa serikali za vyama vya Kiislamu zenye msimamo wa wastani kwa Hamas. "Waisrael lazima watakuwa wamejawa na hasira mbele ya ushindi huu wa Gaza," alisema Abu Waleed, mwenye umri wa miaka 52 huku akisimama miongoni mwa umati unaosubiri kumuona Meshaal, ambaye alinusurika kuuawa na maafisa wa Shirika la ujasusi la Mosad la Israel mwaka 1997 nchini Jordan.

Source News Feed: EMEA Picture Service ,Germany Picture Service Brigedi ya Qassam ya chama cha Hamas wakilinda doria mjini Gaza wakisubiri kuwasili kwa Meshaal.
Brigedi ya Qassam ya chama cha Hamas wakilinda doria mjini Gaza wakisubiri kuwasili kwa Meshaal.Picha: Reuters

Fatah kuhudhuria sherehe ya kuanzishwa kwa Hamas

Mkutano wa leo unasherehekea miaka 25 ya kuanzishwa kwa chama cha Hamas na vuguvugu la kwanza la mapambano ya Wapalestina linalofahamika kama Intifada dhidi ya Israel Desemba 1987. Vita vya hivi karibuni vinatarajiwa kuchukua nafasi kubwa katika,sherehe hii ikionekana katika mfano wa kombora aina ya M75 lililojengwa katika jukwaa la wazi ili kukumbuka maroketi yaliyorushwa mwezi uliyopita kuelekea Tel Aviv na Jerusalem.

Viongozi wa chama cha Fatah katika ukanda wa Gaza wanatarajiwa kuhudhuria sherehe hiyo, hii ikiwa ndiyo mara ya kwanza kwa chama hicho cha rais Mahmoud Abbas kushiriki katika sherehe hiyo tangu mwaka 2007, kilipopigana vita vifupi na Hamas ambapo Hamas iliibuka mshindi. Msemaji wa Hamas Sami Abu Zuhri aliliambia shirika la habari la Reuters, kuwa hotuba ya Meshaal itabainisha vipaumbele vya Hamas katika wakati ujao, na hasa utekelezaji wa maridhiano na Fatah.

Khaled Meshaal akisalimiana na kiongozi wa Fatah, rais wa Palestina mahmoud Abbas.
Khaled Meshaal akisalimiana na kiongozi wa Fatah, rais wa Palestina mahmoud Abbas.Picha: picture-alliance/dpa

Meshaal asisitiza haja ya maridhiano na Fatah

Akifahamu wazi shauku ya Wapaelstina wa kawaida kumaliza migawanyiko ambayo imedhoofisha harakati zao mbele ya jumuiya ya kimataifa, Meshaal alikuwa akirejea mada hiyo ya maridhiano wakati wa mikutano yake yote aliyoifanya mjini Gaza siku ya Ijumaa. "Mwenyezi Mungu akipenda, maridhiano yatafikiwa," alisema, na kuongeza kuwa umoja wa kitaifa ni muhimu wakati alipozungumza mbele ya gofu la nyumba moja iliyoharibiwa katika shambulio la Israel mwezi uliyopita na kuua watu 12, wakiwemo watoto 4.

Lakini ni rahisi kuyazungumzia maridhiano kuliko kuyatekeleza. Wakati Hamas ikichagua njia ya upinzani wa kutumia silaha dhidi ya Israel, Fatah inasema inataka majadiliano na taifa hilo la Kiyahudi. Suala lingine ni kwamba makundi yote mawili yamejikita katika maeneo yao na kila moja lina jeshi lake ambalo hayataki kuyaachia. Katiba ya kwanza ya Hamas inatoa wito wa kuisambaratisha Israel, lakini viongozi wake wamekuwa wakionyesha nia ya kujadili amani ya muda mrefu, kama Israel itakubali kuondoka na kurudisha mipaka iliokuwepo kabla ya vita vya mwaka 1967, wakati Israel ilipoiteka Jerusalem Mashariki, Gaza na ukingo wa Magharibi.

Hata hivyo, Hamas inasema haitalitambua rasmi taifa la Israel, na inachukuliwa kama kundi la kigaidi na Israel, Marekani na serikali nyingi za magharibi. Meshaal ameiendesha Hamas akiwa uhamishoni kuanzia mwaka 2004 hadi Januari mwaka huu kutokana na vita vya rais Bashar al-Assad dhidi ya Waislamu wa Sunni, ambao imani yao na siasa zao ni sawa na Wapalestina. Sasa hivi anatumia muda wake kwenda kati ya Qatar na Misri.

Source News Feed: EMEA Picture Service ,Germany Picture Service Mwanaume wa kipalestina akipeperusha picha ya Khaled meshaal mjini Rafa, katika ukanda wa Gaza.
Mwanaume wa kipalestina akipeperusha picha ya Khaled meshaal mjini Rafa, katika ukanda wa Gaza.Picha: Reuters

Je, ataendelea na mipango yake ya kustaafu?

Awali, kuondoka kwake ghafla kutoka mjini Damascus kulidhoofisha nafasi yake ndani ya Hamas. Uhusiano na utawala mjini Damascus na Tehran ulimfanya kuwa mtu muhimu, lakini kuvunjika au kuharibika kwa uhusiano huo kuliwafanya wapinzani wake mjini Gaza kuanza kuweka mamlaka yao. Licha ya kurejesha ushawishi wake wakati wa vita na Israel, akifanya kazi kwa karibu na serikali ya Misri kuleta makubaliano ya kusitisha vita, anasema anapanga kukaa pembeni katika muda mfupi.

Hamas imekuwa ikiendesha mchakato wa siri wa kumchagua kiongozi mpya kwa kipindi cha miezi sita iliyopita na duru za ndani zinasema mapokezi makubwa aliyoyapata Meshaal katika mitaa ya Gaza yataweka shinikizo kwake kuendelea kuwepo kama kiongozi wa juu wa kundi hilo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre

Mhariri: Sekione Kitojo