1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KHARTOUM: China yaitaka Sudan ilegeze msimamo

9 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCB8

China imeitaka Sudan kulegeza msimamo wake kuhusu pendekezo lililotolewa na katibu mkuu wa zamani wa umoja wa mataifa Kofi Annan juu ya shughuli za kulinda amani katika jimbo Darfur la magharibi mwa Sudan.

Mjumbe wa China Zhai Jun ameeleza kuwa nchi yake inaheshimu juhudi za Khartoum katika kurejesha hali ya utulivu katika jimbo la Darfur lakini wakati huo huo amesema kwamba China inatarajia zaidi kuhusu pendekezo la bwana Annan kutoka kwa serikali ya Sudan.

China ni muwekezaji mkubwa wa kigeni nchini Sudan na jamii ya kimataifa inaitaka nchi hiyo kuutumia uhusiano wake kuishawishi serikali ya Khartoum juu ya mtazamo wake kuhusu jimbo la Darfur.

Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini atazuru Sudan hapo kesho, anatarajiwa kumtolea mwito rais Omar el Bashir juu ya kukubali pendekezo la kupelekwa kikosi cha pamoja cha umoja wa nchi za Afrika na kile cha umoja wa mataifa katika jimbo la Darfur.