1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KHARTOUM: Mazungumzo ya kusaka amani ya Somalia ya mjini Khartoum-Sudan yako hatarini

1 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCx4

Mahakama za kiislamu kutoka Somalia, zimetoa mwito wa kuahirishwa mazungumzo ya kusaka amani na serikali ya mpito ya Somalia ili zichunguzwe taarifa za kuweko majeshi ya kigeni nchini Somalia. Wakati zikifanyika juhudi kubwa kuyanusuru mazungumzo ya amani ya mjini Khartoum nchini Sudan, ujumbe wa mahakama za kiislamu, umesema tume ya uchunguzi ya kimataifa ingeundwa na kupewa muda wa kuchunguza kama Ethiopia na Eritrea kweli zina wanajeshi nchini Somalia.

Mahakama za kiislamu zinapinga kuanzishwe mazungumzo hayo ya mjini Khartoum na serikali ya mpito kabla ya Ethiopia kuyaondoa majeshi yake kutoka Somalia na Kenya itolewe miongoni mwa wapatanishi. Kwa upande wake serikali ya mpito ya Somalia, inailaumu Eritrea kwamba iliwapeleka wanajeshi kiasi ya 2,000 kuwasaidia wapiganaji wa mahakama za kiislamu. Wakati huo huo, wanajeshi wa serikali ya mpito na wapiganaji wa mahakama za kiislamu ambao wametenganishwa na eneo la kilomita 20 tu, wamezusha hofu miongoni mwa raia kwa kufiatua risase na makombora na kupiga mizinga hewani, kila upande ukionyesha nguvu zake.

Mashahidi wamesema wanajiji kadhaa wamekimbia lakini hakuna aliojeruhiwa.