1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Khartoum: Mjumbe wa UM awasili Sudan kuzungumzia Darfur

20 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CChh

Afisa mmoja wa ngazi ya juu anayeratibu uungaji mkono wa Umoja wa mataifa kwa jeshi la umoja wa Afrika katika jimbo la Darfur nchini Sudan, ameanza mazungumzo leo mjini Khartoum. Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Sudan ilisema kwamba Bw Ahmadou Ould Abdullah anakutana na waziri wa nchi anayehusika na mambo ya nchi za nje Ali Karti na anatarajiwa kuonana pia na Rais Omar Hassan al-Bashir baadae leo. Ould Abdullah kutoka Mauritania ni mjumbe aliyeteuliwa na katibu mkuu wa umoja wa mataifa Kofi Annan kuzungumza na serikali ya Sudan juu ya mpango wa awamu tatu kukiimarisha kikosi cha umoja wa Afrika kilichoko Darfur. Akizungumza hapo mapema mjini New York Bw Annan ameelezea matumaini ya kupatikana maelewano. Rais al-Bashir wa Sudan amekataa kabisa kupelekwa wanajeshi wa umoja wa mataifa katika jimbo la Darfur, akizishitumu nchi za magharibi kuwa zina azma ya kuivamia nchi yake. Marekani inayoishutumu serikali ya Sudan kwa mauaji ya raia huko Darfur imetishia kuweka amri inayopiga marufuku urukaji ndege katika anga ya jimbo hilo ikiwa serikali ya Sudan itaendelea kukataa kutumwa jeshi la kulinda amani la umoja wa mataifa.