1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KHARTOUM : Wakubaliana juu ya mzozo wa kusini

3 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/C7AH

Viongozi wa Sudan wamekubaliana juu ya njia ya kuondokana na mzozo mbaya kabisa kuwahi kuwakumba hadi sasa katika utekelezaji wa makubaliano ya amani ya mwaka 2005 yaliokomesha miongo miwili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya kaskazini na kusini mwa nchi hiyo.

Waziri wa serikali ya jimbo la kusini Luka Piong amewaambia waandishi wa habari kwamba Rais Omar Hassan al Bashir amefikia makubaliano na kiongozi wa jimbo la kusini Salva Kiir ambaye ni makamo wa kwanza wa rais hapo jana usiku ambapo vifungu vyote vya makubaliano ya amani vitatekelezwa kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Mawaziri wanaotokea kusini waliojiuzulu nyadhifa zao katika serikali ya umoja wa kitaifa hapo mwezi wa Septemba kupinga kuzorota kwa utekelezaji wa makubaliano hayo watarudi kwenye kazi zao mara baada ya kuchukuliwa kwa hatua zinazohitajika kutekeleza makubaliano mapya.