1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Khodorkovsky apatikana na hatia

Admin.WagnerD27 Desemba 2010

Tajiri mkubwa nchini Urusi, Mikhail Khodorkovsky, amepatikana tena na hatia katika kesi iliyoendeshwa katika Mahakama Kuu mjini Moscow leo (27 Disemba 2010).

https://p.dw.com/p/zqEC
Maandamano mjini Moscow mwanzoni mwa mwezi Disemba 2010
Maandamano mjini Moscow mwanzoni mwa mwezi Disemba 2010Picha: AP

Mashirika ya habari ya ITAR-TASS na Interfax yameeleza kuwa, mahakama hiyo ilimpata Khodorkovsky pamoja na mshitakiwa wake mwenza, Platon Lebedev, na hatia ya ubadhirifu. Watu hao wawili wameshitakiwa kwa pamoja kwa matumizi mabaya ya tani milioni 218 za mafuta kutoka katika kampuni yake binafsi ya Yukos kati ya mwaka 1998 na 2003, madai ambayo kundi lake la mawakali linasema kuwa hayana msingi. Ni waandishi wachache tu waliruhusiwa kuingia katika chumba cha mahakama kwa ajili ya hukumu hiyo na jaji Viktor Danilkin baadaye aliwataka hata hao waandishi wachache kutoka nje ya ukumbi wa mahakama wakati hukumu hiyo ikisomwa.

Khodorkovsky mwenye umri wa miaka 47, ambaye alikuwa ni mtu tajiri sana nchini humo, hivi sasa ni mfungwa maarufu sana, na tayari anatumikia kifungo cha miaka minane kwa madai ya udanganyifu, ambapo waungaji wake mkono wanasema kuwa ni madai ya kupandikizwa na maafisa.

Lakini Khodorkovsky ambaye alitarajiwa kuachiliwa huru mwakani, amefikishwa tena mahakamani kwa madai ya ubadhirifu na kuingiza fedha haramu katika mabenki, ambapo hukumu yake ni kifungo zaidi, na kiongozi huyo wa kampuni kubwa la mafuta ambalo limevunjwa la Yukos , atabakia jela hadi mwaka 2017.

Kufuatiliwa kwa Khodorkovsky kumekuwa hatua yenye utata kabisa ya kisheria katika enzi za tangu kuvunjika kwa Urusi ya zamani.

Waungaji mkono wa Khodorkovsky wanamuona kama mhanga na shahidi ambaye anaadhibiwa kwa kujaribu kumpinga kiongozi mwenye nguvu nchini humo Vladimir Putin kwa kuvifadhili vyama vya upinzani, lakini maafisa wa Urusi wanamuona kuwa ni fisadi ambaye amenufaika kwa kuvunja sheria.

Rais Dmitry Medvedev amesisitiza kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria nchini Urusi, akisisitiza kuwa si rais ama afisa yeyote wa serikali ambaye ana haki katika suala hili kuamua kinyume na uamuzi uliotolewa, awe hana hatia ama ana hatia. Hii lazima ieleweke.

"Iwapo ushahidi utapatikana dhidi ya mtu mwingine yeyote ni lazima utolewe. Kwa kuwa ushahidi huo haupo, mtu anaweza kufikiri, kuwa mahakama inachagua katika kutoa haki." Amesema Medvedev.

Mamia ya waandishi habari pamoja na waungaji mkono wa Khodorkovsky walijazana katika mahakama hiyo mjini Moscow, na wakashangaa kugundua kuwa hakuna matangazo ya hukumu ya kesi hiyo katika chumba cha waandishi wa habari.

Hukumu ya kesi hiyo iliangaliwa kuwa kama kigezo muhimu cha mwelekeo wa hapo baadaye wa Urusi chini ya waziri mkuu Putin na rais Dmitry Medvedev, huku kukiwa na uvumi kuwa Putin ana panga kurejea tena katika kiti cha urais katika uchaguzi wa mwaka 2012.

Mwandishi: Sekione Kitojo /AFPE/DPAE

Mhariri: Josephat Charo