1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kibaki aapishwa kipindi cha pili cha urais Kenya

31 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CiH5

NAIROBI

Rais Mwai Kibaki wa Kenya ameapishwa kwa kipindi cha pili madarakani kufuatia ushindi katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo ambao mpizani wake mkuu Raila Odinga amepinga matokeo yake kwamba yametokana na uporaji mkubwa wa kura.

Samuel Kivuitu Mkuu wa Tume ya Uchaguzi nchini Kenya alkitangaza matokeo ya uchaguzi huo amesema Kibaki amejipatia kura 4,584,721 wakati Odinga amejipatia kura 4,352,993.

Mgombea alieshindwa katika uchaguzi huo Raila Odinga kwa takriban kura 200,000 ametowa wito kwa wafuasi wake kupinga kuchaguliwa tena kwa Kibaki kutokana na kile alichosema wizi mkubwa wa kura na kufuatia ghasia zilizozuka baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo polisi imefyetuwa risasi na kuuwa watu saba.

Katika hotuba ya kuapishwa kwake Rais Kibaki ametowa wito wa kuwepo kwa usuluhishi wa kitaifa.

Kibaki amesema akiwa Rais wa Kenya atamtumikia kila mtu kwa haki bila ya kujali amempigia kura nani na amewataka wananchi wote kuweka kando hamasa zao zilizotokana na mchakato wa uchaguzi na kushirikiana kama ni watu wa aina moja kwa dhamira moja ya kujenga nchi madhubuti yenye umoja,ustawi na haki.

Mara tu baada ya kuapishwa kwake serikali ya Kenya imepiga marufuku repoti zote zinazotolewa hewani moja kwa moja na radio na televisheniaza nchi hiyo wakati ghasia zikienea nchi nzima kufuatia kutagazwa kuchaguliwa tena kwa Kibaki kuwa rais wa nchi hiyo.