1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kibaki achaguliwa tena kuwa Rais Kenya

30 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CiBI

NAIROBI.Rais Mwai Kibaki ametangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi mkuu wa Kenya, baada ya kumshinda mpinzani wake Raila Odinga wa Chama cha ODM kwa zaidi ya kura laki mbili.

Lakini wakati tume ikitangaza matokeo hayo mjumbe mmoja katika tume ya uchaguzi nchini humo ametangaza kujitoa katika tume hiyo kwa kile alichodai kukataa kujihusisha na wizi wa kura.

Mjumbe huyo Kipkemoi Arap Kirui katika mkutano na waandishi wa habari muda mfupi uliyopita, amesema kuwa alikataa kutia saini katika fomu za matokeo ambazo ziligushiwa na kwamba imani yake haimtumi kuendelea akubaki ndani ya tume hiyo.

Mapema Mwenyekiti wa tume hiyo Samwel Kivuitu alitangaza matokeo baada ya kupitia upya fomu zilizowasilishwa, ambapo ilionesha kuwa Rais Mwai Kibaki alikuwa mbele kwa kura chache dhidi ya hasimu wa Raila Odinga.Katika matokeo ya awali Raila alikuwa mbele.

Uhesabuji kura ulisitishwa wakati ambapo tume ya uchaguzi nchini humo ikipitia upya baadhi ya matokeo.

Raila alikuwa akiongoza kwa wingi mkubwa wa kura dhidi ya Rais Kibaki. Lakini katika matokeo yaliyotangazwa jana na tume ya uchaguzi, mwanya wa kura hizo ulipungua ambapo Raila alikuwa mbele kwa kura elfu 38 dhidi ya Rais Kibaki.

Kuchelewa kutolewa kwa matokeo hayo kumepelekea ghasia ambapo inaarifiwa ya kwamba watu wanane wameuawa katika ghasia hizo.

Mapema vyama vyote viwili kile cha Rais Kibakai cha PNU na ODM vilidai kupata ushindi katika uchaguzi huo.