1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kifo cha Gaddafi ni mwanzo wa kipindi kipya Libya

21 Oktoba 2011

Kifo cha dikteta wa Libya Muammar Gaddafi kinaashiria mwanzo wa kipindi kipya cha kihistoria nchini Libya. Kwa maoni ya mwandishi wetu Rainer Sollich, nchi hiyo inakabiliwa na changamoto kali kweli.

https://p.dw.com/p/12wKe
Wananchi wa Libya wakishangilia kifo cha GaddafiPicha: picture-alliance/dpa

Muammar Gaddafi katika hotuba yake ya ajabu kwenye televisheni, aliwaita raia walioasi kuwa ni "panya". Sasa watu hao waliokuwa wakipigania uhuru wao, wamemuua katika mapigano yaliyozuka. Muammar Gaddafi amefariki alipojaribu kukimbia kutoka Sirte, ngome mwisho ya wafuasi wake, ambayo muda mfupi kabla ilitekwa na wapinzani wa dikteta wa Libya. Ionekanavyo, kiongozi huyo wa zamani aliekuwa na miaka 69 ameuliwa katika kitendo cha kujitwalia sheria. Amekufa kama alivyowahi kuashiria kuwa atapigana mpaka kufa humo humo nchini.  Ulimwengu ulipokuwa ukiuliza iwapo amefariki au amekamatwa tu, watu wenye furaha walianza kufyatua risasi katika mji mkuu Tripoli.

Nchini Libya na hata katika ulimwengu wa Kiarabu ni wachache wanaomlilia. Na nchi za magharibi ndio kabisa, kwani Gaddafi hakuchukuliwa tu kama mtu aliefadhili ugaidi na kuyashinikiza mataifa kupata maslahi yake bali kwanza kabisa alitazamwa kama ni mpinzani wa kijeshi. Hata hivyo Muammar Gaddafi aliweza kupiga kambi mjini Brussels na Paris kwa shangwe kubwa kwa sababu ya ukiukaji kadhaa wa mashaka na dosari ya mwongozo wa haki za binadamu katika sera za nje za Umoja wa Ulaya. Alikaribishwa na wanasiasa wa Umoja wa Ulaya na alitumia njia za mashaka kuwazuia wakimbizi wa Kiafrika kwenda nchi za Ulaya. Marekani na nchi za Ulaya zilianza kubadili sera hiyo mpya ya kukaribiana nae, baada ya watu wa Libya kuanza kuasi dhidi ya kiongozi wao.

Muammar al Gaddafi / Libyen
Muammar Gaddafi alikuwa kiongozi wa Libya kwa miaka 42Picha: dapd

Hata kama nchi za magharibi hatimae zimechangia kijeshi kuleta mageuzi nchini Libya, yote hayo hayapaswi kusahauliwa - na mafunzo dhahiri yapatikane juu ya namna ya kukabiliana na madikteta katika siku zijazo. Mpaka sasa Umoja wa Ulaya ulikuwa ukijizuia kutamka lo lote.

Kifo cha Gaddafi kinawaondoshea Walibya mzigo mkubwa katika maisha ya siku zijazo. Miwsho wake ni dalili kwamba enzi mpya inaanza kweli hivi sasa, katika nchi hiyo ya jangwani ya Afrika Kaskazini yenye utajiri wa mafuta . Changamoto za kisiasa ni kubwa kupita kiasi. Libya haina uzoefu wa mfumo wa kisiasa wala taasisi za kiserikali zinazofanya kazi. Mtu anaweza kusema, nchi hiyo ndio kwanza inachipuka. Viongozi wa serikali ya mpito wanapaswa kutayarisha uchaguzi wa kidemokrasia na wakati huo huo kuyaleta pamoja makundi hasimu ya kikabila na makundi ya kisiasa ya nadharia mbali mbali. Libya haiwezi kuyatekeleza hayo yote peke yake. Libya yenyewe inapaswa kutafuta njia yake lakini itahitaji msaada wa kimataifa. Na wala isione haya kuchukua msaada huo.

Mwandishi: Rainer Sollich/ZPR

Tafsiri: Prema Martin

Mhariri: Mohammed Khelef