1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiir avunja baraza la mawaziri

24 Julai 2013

Ulinzi mkali umeimarishwa katika taasisi muhimu za serikali mjini Juba, wakati matangazo ya redio yakitoa wito wa kuwepo utulivu baada ya rais Salva Kiir kulivunja baraza lake la mawaziri.

https://p.dw.com/p/19DUV
Rais wa Sudan, Salva Kiir
Rais wa Sudan, Salva KiirPicha: picture-alliance/dpa

Wanajeshi wa Sudan Kusini pamoja na polisi wameimarisha ulinzi katika taasisi muhimu za serikali katika mji mkuu Juba, wakati matangazo ya redio yakitoa wito wa kuwepo utulivu baada ya rais Salva Kiir kulivunja baraza lake la mawaziri.

Makamu wa rais ni miongoni mwa waliofutwa kazi, hayo yakiwa ni mabadiliko makubwa kuwahi kufanyika katika historia ya nchi hiyo changa yenye miaka miwili.

Taarifa ya Rais Kiir, iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa jana Jumanne jioni, ilieleza kuwa mawaziri wake wote wamefukuzwa kazini na majukumu yao yatafanywa na makatibu wao.

Akizungumza na shirika la habari la AFP, aliyekuwa waziri wa habari na msemaji wa serikali ya Sudan Kusini, Barnaba Marial Benjamin, amesema mawaziri wengi waliofukuzwa kazini walikuwa wanachama muhimu katika chama tawala cha Sudan People's Liberation Movement-SPLM. Mawaziri wote 29 wamefukuzwa, pamoja na manaibu wao na polisi 17 wenye cheo cha Brigedia.

Aliyekuwa makamu wa Rais wa Sudan Kusini, Riek Machar
Aliyekuwa makamu wa Rais wa Sudan Kusini, Riek MacharPicha: Stan Honda/AFP/Getty Images

Mbali na baraza la mawaziri kuvunjwa, Rais Kiir, pia amemfukuza kazi makamu wa rais wa nchi hiyo, Riek Machar, ambaye amewataka wafuasi wake kuwa watulivu. Aidha, kiongozi huyo wa Sudan Kusini, ameamuru uchunguzi ufanyike dhidi ya katibu mkuu wa chama chake tawala cha SPLM, Pagan Amum. Amum alikuwa mjumbe wa juu katika mazungumzo ya kutatua mzozo kati ya Sudan Kusini na Sudan.

Ulinzi mkali waimarishwa

Ulinzi mkali umeimarishwa, baada ya wanajeshi na askari polisi wenye silaha kusambazwa kwenye taasisi za serikali na mitaa ya mji mkuu wa Juba, ingawa hali ilionekana kuwa ya utulivu. Hata hivyo, balozi mbalimbali zimewaonya raia wake kuwa makini. Ubalozi wa Uingereza umewasihi raia wake kubakia nyumbani au kukaa kwenye maeneo salama.

Mwezi uliopita, Rais Kiir aliwafukuza kazi mawaziri wawili muhimu katika serikali yake na alianzisha uchunguzi dhidi ya tuhuma za kashfa za rushwa za mamilioni ya Dola. Hatua hiyo ya Rais Kiir, imewafanya wanadiplomasia wa mataifa ya Magharibi kuwa na wasiwasi huenda Sudan Kusini ikatumbukia katika hali ya kukosekana kwa utulivu, wakati huu ambapo inakabiliana na changamoto mbalimbali, likiwemo suala la kusafirisha mafuta na kuongezeka kwa ghasia za kikabila na waasi.

Marais wa Sudan na Sudan Kusini, Omar Hassan al-Bashir na Salva Kiir
Marais wa Sudan na Sudan Kusini, Omar Hassan al-Bashir na Salva KiirPicha: Reuters

Akihojiwa hivi karibuni, Machar aligusia kwamba huenda akagombea nafasi ya uongozi wa SPLM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Kwa upande wake, Amum alimkosoa Kiir kwa kuwafukuza mawaziri wawili kwa tuhuma za kuhusika na rushwa. Kamati kuu ya chama cha SPLM, imesema itamchunguza Amum.

Hata hivyo, bado haijafahamika mara moja ni lini Rais Kiir ataliteua baraza jipya la mawaziri. Inaelezwa kuwa, baadhi ya mawaziri wamepata taarifa za kufukuzwa kazi kupitia taarifa ya habari kwenye televisheni, huku wengine wakipewa taarifa hizo na mashirika ya habari ya kimataifa kama vile Reuters.

Sudan Kusini ambayo ilijipatia uhuru wake kutoka kwa Sudan, Julai mwaka 2011, hivi karibuni imekifunga kiwanda chake cha mafuta, baada ya Sudan kusema kuwa itayafunga mabomba mawili ya kusafirisha mafuta yaliyoko eneo la mpakani, hadi hapo Sudan Kusini itakapoacha kuwaunga mkono waasi walioko kwenye ardhi ya Sudan Kaskazini.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE
Mhariri:Yusuf Saumu