1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiir na Bashir wajizatiti kutafuta maelewano kati ya Kusini na kaskazini Sudan

18 Oktoba 2007

Kiongozi wa kusini mwa Sudan Salva Kiir na rais Omar El Bashir wamekutana leo hii mjini Khartoum katika juhudi za kusaka suluhu ya mzozo unaotishia kuigawa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/C77g

Mazungumzo ya leo yanategemewa kumfanya kiongozi wa kusini mwa Sudan alishawishi kundi lake lililokuwa zamani la waasi kujiunga tena na serikali ya Umoja wa kitaifa ambayo walijitoa wiki iliyopita.

Mkutano huo umefanyika katika makao ya rais mjini Khartoum ikiwa ni siku moja baada ya rais El Bashir kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri ili ilivyopendekeza serikali ya upende wa Kusini.

SPLM liliwaondoa watu wake katika baraza la mawaziri mnamo Oktoba 11 kufuatia kile walichokitaja ni kushindwa kwa serikali ya mjini Khartoum kutekeleza makubaliano ya amani ya mwaka 2005 kati ya kaskazini na kusini mwa Sudan makubaliano ambayo yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenye vya muda mrefu kabisa katika eneo hilo.

Kundi hilo linadai wanajeshi wa serikali ya Khartoum waondoke kusini na suala la hatma ya jimbo la mafuta linalozozaniwa la Abiye litatuliwe masuala ambayo hadi sasa hayajatekelezwa.

Maelfu ya wanajeshi wa upande wa kaskazini mwa Sudan bado wako Kusini licha ya kumalizika muda uliowataka waondoke eneo hilo july 9 kama ilivyokubaliwa katika mapatano ya amani ya CPA.

Kwa upande wake chama cha rais Omar El Bashir cha national Congress Party NCP kinawalaumu wanachama wa SPLM kwa kuchukua muda mrefu katika kutekeleza makubaliano hayo ya amani ya mwaka 2005.Duru zilizokaribu na rais zimeliambia shirika rasmi la habari la Sudan SUNA kwamba mawaziri wapya walioteuliwa jumatano wanaapishwa leo ili kufungua njia ya kufikiwa suluhu katika mzozo huu mpya ambao umetajwa kuwa mbaya zaidi tangu kusainiwa makubaliano ya amani ya CPA.

Ingawa mkutano wa leo kati ya El Bashir na Kiir unategemewa unaweza kuzuia mzozo usipanuke zaidi tayari katibu mkuu wa chama cha SPLM Bagan Amon ameshasema mawaziri wa kusini hawatajiunga na serikali hadi pale vifungu vilivyoko kwenye makubaliano hayo ya amani ambavyo havijatekelezwa vitakapoanza kutekelezwa.

Aidha SPLM hakijaridhika na mabadiliko yaliyofanywa katika baraza la mawaziri kinadai mapendekezo yao yote hayakuzingatiwa licha ya kwamba El Bashir alimuondoa Lam Akol kwenye wadhifa wa waziri wa mambo ya nje kwa sababu SPLM kinamuona kuwa mtu wa karibu wa chama tawala cha NCP na mtetezi mkubwa wa vitendo vya Serikali katika jimbo tete la Darfur.Wadhifa huo umepewa Deng Alor kiongozi mkuu wa SPLM.

Duru zinasema mivutano imeongezeka kwa muda wa miezi kadhaa sasa kati ya chama hicho cha SPLM cha kusini mwa Sudan na chama tawala cha NCP.Lakini akizungumza hivi karibuni rais Omar El Bashir alisema hawatarudi tena kwenye mapigano na upande wa kusini na makubaliano ya amani ya CPA lazima yaheshimiwe.