1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiir:Makubaliano ya nchi za Sudan yatekelezwe haraka

26 Januari 2013

Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir ametaka kufanyika utekelezaji wa haraka wa makubaliano kadhaa yaliyosainiwa na nchi hasimu ya Sudan na amekosoa hatua ya Sudan kukwamisha mazungumzo kati ya nchi hizo.

https://p.dw.com/p/17RsP
Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir
Rais wa Sudan Kusini, Salva KiirPicha: picture alliance / ZUMA Press

Akizungumza katika mkutano wa usalama mjini Addis Ababa, Ethiopia, Rais Kiir amesema ni lazima waache maneno matupu na kuanza kufanya vitendo. Kiir na rais mwenzake wa Sudan, Omar Hassan al-Bashir, walikutana mapema jana Ijumaa kwa mazungumzo ya ana kwa ana katika hatua ya kushinikiza utekelezwaji wa makubaliano yaliyokwama ya kiuchumi, mafuta na usalama, yaliyosainiwa mwezi Septemba mwaka jana, baada ya kuzuka kwa mzozo katika eneo la mpakani mwaka uliopita.

Masuala mengine yaliyokwama

Masuala mengine muhimu ambayo bado hayajatatuliwa tangu Sudan Kusini ijipatie uhuru wake Julai mwaka 2011, ni pamoja na mkoa wenye mgogoro wa Abyei, pamoja na kuratibu uchimbaji wa mafuta. Jopo la upatanishi la Umoja wa Afrika-AUHIP limewasilisha azimio kuhusu Abyei, ambalo linajumuisha kura ya maoni inayowapa uwezo kabila la Dinka linaloishi Abyei, haki ya kupiga kura sambamba na raia wengine wa Sudan.

Ramani ya mkoa wa Abyei
Ramani ya mkoa wa Abyei

Rais Kiir ameitaka Sudan kuzingatia pendekezo la Umoja wa Afrika kuhusu Abei kwa lengo la kumaliza mgogoro uliodumu kwa muda mrefu sasa. Amesema suala la Abyei ambalo limedumu kwa miaka saba sasa, halihitaji tena majadiliano, bali kinachotakiwa ni kutekelezwa kwa azimio la umoja huo. Akijibu swali iwapo kuna mafanikio yoyote kutokana na mazungumzo yake na Rais Bashir, Rais Kiir amesema bado hawajamalizana.

Lamamra auzungumzia mzozo wa Sudan

Aidha, Kamishna wa Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika, Ramtane Lamamra amesema umoja huo una wasiwasi kwamba tofauti kubwa bado imebakia kati ya mataifa hayo mawili hasimu. Lamamra amezitaka nchi hizo kushinikiza upatikanaji wa muafaka katika kutekeleza makubaliano hayo yaliyokwama. Sudan na Sudan Kusini zimekuwa zikitupiana lawama, ambapo Sudan imeishutumu Sudan Kusini kwa kuwafadhili waasi wa Sudan, jambo ambalo limesababisha kushindwa kutekelezwa kwa makubaliano hayo. Ama kwa upande wake, Sudan Kusini inaishutumu Sudan kwa kuwaunga mkono wanamgambo nchini humo, ikiwa ni njama iliyoitumia kufanya mashambulizi wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miongo miwili.

Rais Kiir na Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan
Rais Kiir na Rais Omar Hassan al-Bashir wa SudanPicha: KHALED DESOUKI/AFP/Getty Images

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE
Mhariri: Sekione Kitojo