1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa chaanza

Admin.WagnerD19 Septemba 2017

Kikao hicho cha baraza kuu la umoja wa Mataifa kimeanza huku mambo yatakayomulikwa zaidi ni pamoja na mgogoro wa Korea Kaskazini, Myanmar na mabadiliko ya tabia nchi.

https://p.dw.com/p/2kGYE
Donald Trump  New York Antonio Guterres UN
Picha: Reuters/L.Jackson

Mambo  yanayomulikwa zaidi katika kikao cha mwaka huu ni mgogoro wa  silaha za nyuklia wa Korea Kaskazini,  mauaji ya waislamu Myanmar na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.

 Baraza hilo la siku sita, linafunguliwa leo  huku  Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa , Antonio Gutteres akitarajiwa kutoa hotuba yake ikiwa ni mara yake ya kwanza kuhudhuria baraza hilo.

 Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni  Gutterres alisema kikubwa atakachozungumza katika baraza hilo ni mgogoro wa Korea Kaskazini, mgogoro wa Myanmar na  mabadiliko ya tabia nchi.  Alisema mgogoro wa Korea Kaskazini ni miongoni mwa changamoto kubwa inayoikabili dunia kwa sasa.

 Ingawa Rais wa China Xi Jinping hatahudhuria baraza hilo lakini Rais Trump alizungumza naye kwa njia ya simu kuhusu ulazima wa kulitumia baraza la usalama la umoja wa mataifa  kutafuta suluhu kwa kuishinikiza Korea Kaskazini kuacha matumizi ya silaha za kinyuklia.

Nordkorea Wahlen 2015 Kim Jong Un
Kikao cha baraza Kuu la Umoja wa Mataifa litajadili kwa mapana mzozo wa Korea KaskaziniPicha: picture-alliance/dpa/R. Sinmun

Kadhalika katika mkutano huo, viongozi wengi wanahofia kuhusu nafasi na wajibu wa Marekani duniani na watapata nafasi ya kukutana na kumsikia Donald Trump ambaye anatajwa kuwa ni mgeni katika masuala ya kidiplomasia.

Pia hotuba yake inatarajiwa kuupiga zaidi Umoja wa Mataifa kwani tayari katika hotuba zake za awali mara baada ya kufika New York ameanza kuuponda akisema kuna urasimu na kurejea wito wake wa kufanyika mageuzi.

Kwa mujibu  wa ratiba ya baraza hilo, mara baada  ya Gutteres kutoa hotuba yake ya ufunguzi, atafuatia Rais wa Brazil, Michel Temer na baadaye Donald  Trump.

Wengine watakaohutubia ni pamoja na Mfalme wa Qatar  Sheikh Tamin bin Hamad Al-Thani ambaye nchi yake inatuhumiwa kushirikiana na makundi ya kigaidi, wengine ni Rais wa Uturuki, Recep Tayip  Edrogan na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Mada nyingine zinazotarajiwa kujadiliwa katika baraza hilo ni migogoro katka nchi za Venezuela, na Syria na mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi kama  al-Qaida na  Dola la Kiislamu.

Mwandishi: Florence Majani, AFP,AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman