1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kikao cha mwaka cha baraza kuu la Umoja wa mataifa:Viongozi wazungumzia kupanda bei za vyakula.

24 Septemba 2008

Wasema kunaathri hatua za kufikia malengo ya milenia.

https://p.dw.com/p/FO4S
Wajumbe katika ukumbi wa Baraza kuu la Umoja wa mataifa mjini New York.Picha: AP

Kikao cha mwaka huu cha baraza kuu la Umoja wa mataifa, kimegubikwa na masuala kadhaa . Miongoni mwa masuala makuu ni kupanda kwa bei za vyakula duniani, jambo ambalo viongozi wakuu wa mataifa masikini duniani wanasema ni mzigo mkubwa kwao. Kutokana na hayo wametoa wito zichukuliwe hatua za kivitendo kuubadili mkondo huo ambao unahatarisha ukuaji uchumi .

Athari za kupanda mno kwa bei za vyakula ni jambo lililozungumzwa katika hotuba za viongozi wanaokusanyika katika kikao cha mwaka cha baraza kuu la umoja wa mataifa mjini New York, ambako wajumbe wanatathimini jinsi mataifa wanachama yanavyoendelea na jitihada za kufikia malengo ya milenia ya umoja huo ikiwa ni pamoja na kupunguza kiwango cha umasikini kwa nusu ifikapo 2015.

Rais Marc Ravalomanana wa Madagascar alisema " mzozo wa sasa wa chakula ni mzigo mzito na unazusha changamoto nyingi mpya." Akazikosoa nchi tajiri za viwanda kwa utaratibu wa kufidia wakulima wao kwa ruzuku, jambo ambalo limeiathiri sekta ya kilimo katika nchi zinazoendelea.

Rais huyo wa Madagascar akasema hasa nchi za kiafrika, zitashindwa kuondoa umasikini ikiwa bei za vyakula zitabakia kuwa za juu, na akazitaka nchi tajiri zitekeleze ahadi zao kwa nchi masikini, zinazojitihadi kukabiliana na tatizo la kupanda kwa bei.

Rais Mwai Kibaki wa Kenya alisema bei za vyakula zimeongezeka duniani kote, lakini athari zake ni kubwa zaidi katika nchi zinazoendelea ambako ndiko inakoishi sehemu kubwa ya walio masikini duniani. Akaongeza," kuendelea kupanda bei za vyakula kuna athari zake katika usalama wa taifa, katika mataifa mengi yanayoendelea.

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika amesema " bei za juu za vyakula pamoja na msukosuko katika masoko ya fedha,yanatia wasi wasi." Akasema kuna haja ya kuchukuliwa hatua kabambe kusawazisha hali hiyo na kuitaka jumuiya ya kimataifa na wadau wengine wanaohusika na uchumi wa dunia wachukue hatua za haraka. Akiuomba umoja wa mataifa uchukuwe uongozi.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon aliwaambia wajumbe wa nchi 198 wanachama kwamba katika kipindi cha mwaka mmoja bei za vyakula msingi ambavyo ni lishe kwa nusu ya wakaazi wa dunia zimepanda zaidi ya mara mbili

Wakati bei za baadhi ya vyakula vya msingi zimeshuka kwakiasi fulani baada ya kupanda mwezi Juni, lakini bado ni za juu kwa asili mia 44 ikilinganishwa na hali ilivyokua 2006.

Benki ya dunia imeonaya kwamba watu 100 milioni zaidi wanaweza wakasukumwa katika umasikini kwa sababu ya kupanda bei za vyakula na mafuta mambo ambayo yamesababisha pia kuongezeka bei ya mbolea.

Mikutano ya maafisa kandoni mwa mkusanyiko huo katika baraza kuu la umoja wa mataifa, imetuwama katika njia za kuirekebisha hali ya mambo, huku mashirika ya maendeleo na misaada ya kimataifa yakiomba fedha zaidi kusaidia kuzipa msukumo bei za vyakula katika nchi zinazoendelea.