1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kikulacho kinguoni mwako!Magaidi walitokea ndani!

Abdu Said Mtullya7 Julai 2010

Leo umetimu mwaka wa tano tokea kufanyika mashambulio ya mabomu jijini London.

https://p.dw.com/p/ODSf
Maombolezo ya watu walioangamizwa na magaidi mjini London, miaka mitano iliyopita.Picha: AP

Leo umetimia mwaka wa tano tokea watu zaidi ya 50 waangamizwe kutokana na mashambulio ya mabomu katika treni na mabasi jijini London.

Mamia wengine walijeruhiwa katika mashambulio hayo yaliyofanywa na magaidi wazaliwa wa ndani ya nchi za Ulaya.Jee vipi jamii zinaweza kujihami dhidi ya magaidi wa aina hiyo?

Siku kama ya leo miaka mitano iliyopita,magaidi walifanya mashambulio ya mabomu katika treni ya chini ya ardhi na katika mabasi jijini London.

Watu 56 waliuawa na wengine zaidi ya mia saba walijeruhiwa. Mashambulio hayo hayakufanywa na watoka mbali, bali na magaidi waliozaliwa na kukulia katika nchi za Ulaya- tunaoweza kuwaita magaidi wa ndani.

Mashambulio kama hayo pia yalifanyika mnamo mwaka 2004 katika vyombo vya usafirishaji wa umma katika mji wa Madrid. Watu 191 waliuawa na wengine 1460 walijeruhiwa. Waliofanya mashambulio hayo pia walikuwa magaidi waliotokea ndani.

Nchini Ujerumani vile vile magaidi wa kundi linaloitwa "Sauerland" walipanga kuripua mabomu.

Jee nchi za Ulaya zina mkakati wa kukabiliana na hatari ya magaidi wanaotokea ndani ya nchi? Magaidi hao wanaotokea ndani wanatafautiana na wale waliofanya mashambulio ya tarehe 11 mwezi septemba nchini Marekani.

Magaidi hao wa ndani walikulia katika nchi hizo ambamo walifanya mashambulio. Walisoma katika shule za nchi hizo. Na wengi wao wanatoka katika familia zisizokuwa na nasaba za kidini zenye kina kirefu na wala hawakukuzwa katika malezi yaliyofuata mwelekeo mkali wa kidini.Watu hao walikubalika katika jamii , hadi hapo walipoanza kuwa na mawasiliano na wanaitikadi kali wa Kiislamu.

Baadhi ya magaidi hao wala hawakuwamo katika familia zilizokuwa na nasaba za kiislamu. Lakini walisilimu baadae katika maisha yao.

Funzo mojawapo muhimu ambalo Uingereza ililipata baada ya mashambulio ya jijini London, ni kujaribu kuepusha kuigawa jamii. Hayo ameyasema Magnus Ranstorp wa chuo cha masuala ya usalama cha mjini Stockholm.Amesema idara mpya ya Scotland Yard ilifanikiwa kutoa habari kwa kauli moja.

Polisi walijitahidi kuileta jamii pamoja.Lakini pia ni muhimu kwa idara za usalama kushirikiana na wananchi katika jumuiya zao kwani ni katika jumuiya hizo ambamo magaidi wanatokea.Hayo ameyasisitiza naibu waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Ole Schröder.

Hatua nyingine muhimu ni kujenga mawasiliano na vijana wa Kiislamu kabla hawajatiwa kwenye siasa kali. Na kwa ajili hiyo elimu kwa maimamu inaweza kutoa mchango mkubwa. Wanahitajika maimamu wanaotoa mawaidha ya dini na siyo wale wanaoneza chuki. Hatua hiyo imeshachukuliwa nchini Uhispania na Uingereza. Idara zinazohusika zinashirikiana na jumuia za Waislamu,misikiti na maimamu ili kuepusha mawasiliano baina ya vijana wa Kiislamu na makundi ya itikadi kali.

Mwandishi/Schmidt Fabian/ZA

Tafsiri:Mtullya Abdu

Mhariri: Miraji Othman