1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kila mmoja adai Spain ndio mabingwa wapya wa dunia ?

11 Julai 2010

Na je, Paul na Pauline wasemaje ?

https://p.dw.com/p/OFXf
Spain-mabingwa wapya wa dunia ?Picha: AP

Wakati Ujerumani ina miadi na Uruguay leo usiku kuania mshindi watatu, wapiga-ramli wote na mashabiki wa dimba wadai Spain na sio Holland ndiyo itakayotawazwa bingwa mpya wa dunia hapo kesho huko City Stadium,Johannesberg.

Pweza wa Ujerumani- Paul- ametabiri Spain ndio mabingwa wakati mkewe- Pauline , ameelemea timu ya nyumbani Holland. Nani kati yao atashinda finali hii kati ya Spain na Holland na Paul na Pauline ?

Kuanzia watoto wa shule huko Soweto, Afrika Kusini, hadi vituo vya kamari ulimwenguni na hata pweza-dume, Paul wa Oberhausen , Ujerumani, upatu unapigwa na kuhanikiza Kombe la dunia kesho Jumapili linakwenda Spain, Na hiyo itakuwa mara ya kwanza .

"Wanacheza dimba maridadi ajabu.Tunataka kuwa kama wao. Bila shaka, watashinda Jumapili hii- fanyeni hivyo Spain."-alisema shabiki chipukizi wa miaka 13, Dumisani Motye, aliekuwa akimuigiza David Villa wa Spain katika uwanja wa vumbi mtaani Soweto.

Kabla ya changamoto hiyo, Ujerumani na Uruguay zitateremka uwanjani huko Port Elizabeth leo usiku kuamua finali ndogo ya Kombe la dunia mwaka 2010: Nani ni mshindi wa tatu ? Baada ya kumaliza wapili mwaka 2002 na watatu nyumbani mwaka 2006, Ujerumani leo haitaki chochote kasoro ya taji hilo la mshindi watatu kufuta machozi ya pigo la pweza Paul,alieangusha juzi kwa kutabiri ushindi wa Spain.

Lakini, Waspain, waliopigiwa debe tangu mwanzo kuwa ndio mabingwa wapya wa dunia, baada ya kuanza taratibu wamepata kasi wakati muwafaka-hatua za mwisho za kombe hili baada ya kuwaambia Wajerumani,kutangulia si kufika. Nani sasa atazuwia "kikosi cha manuwari za Spain" kutia gati bandarini City Stadium?

Manahodha wa Holland pia ni maarufu na wanadai ni jahazi la kocha Bert van Marwijk lililowafungisha virago mabingwa mara tano, Brazil, seuze Waspain.

Kama Spain, Holland, haikuwahi kutwaa kombe la dunia na mara hii, wanataka kufuta madhambi ya 1974 na 1978 walipofika finali na kupokonywa Kombe na Ujerumani na Argentina. Wanadai, halali ni mara tatu.

Vyovyote mpambano wa kesho utakavyomalizika, jina jipya litaandikwa katika Kombe la FIFA. Isitoshe, utakuwa ushindi wa kwanza wa timu ya Ulaya wa Kombe la dunia nje ya bara lao.

Na sura hii haikuonesha hivyo pale firimbi ilipolia Juni,11 kuanzisha kombe la kwanza la dunia barani Afrika. Kwani,timu za kanda ya Amerika kusini,zilitia fora ,lakini mwishoe, ilidhihirika vishindo vyao vilikuwa vya darini vilivyoishia sakafuni. Na hii, licha ya mabingwa wa dunia, Itali, makamo-bingwa ,Ufaransa na England, mabingwa 1966 kuanguka. Hata Spain, utakumbuka ilishindwa mpambano wake wa kwanza na Uswisi.

Holland, haikufungwa hata mechi moja katika Kombe hili la dunia na mpambano wa kesho utakuwa wa 14 mfululizo bila kushindwa.

Hizo ni salamu akina Arjen Robben, van Marwijk, van Bommel, van der vaart, van Persie na van Brockhorst wanazompelekea Del Bosco na La Roja,timu yake ya Spain.

Wakati salamu za pweza "Paul" kutoka Ujerumani kuwa ni Spain itakayoshinda kesho, amezipokea mkewe "Pauline" huko The Hague,Holland, mashabiki wa Afrika kusini,wanadai Wadachi-Holland, asili ya makaburu, wamerudi nyunmbani, na mcheza kwaohutunzwa-Pauline amkumbusha pweza Paul.

Mwandishi: Ramadhan Ali/RTRE

Uhariri: Miraji Othman