1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kim Jong Ill azikwa

Caro Robi28 Desemba 2011

Korea Kaskazini imekamilisha mazishi ya kiongozi wake marehemu Kim Jong Il yaliyochukua saa tatu, huku gari lililobeba jeneza lake likirejea katika kasri ambapo mwili wa kiongozi huyo utahifadhiwa.

https://p.dw.com/p/13aWj
Kim Jong Un, mwana na mrithi wa urais wa Korea Kaskazini, akisindikiza mwili wa baba yake, Kim Jong Ill.
Kim Jong Un, mwana na mrithi wa urais wa Korea Kaskazini, akisindikiza mwili wa baba yake, Kim Jong Ill.Picha: AP

Maelfu ya wanajeshi na raia wamejitokeza katika barabara za mji wa Pyongyang ambapo msafara uliobeba mwili wa kiongozi wao, Kim Jong Ill, ulipitia.

Licha ya baridi kali na theluji kuanguka, waomboezaji hao walijitokeza kwa wingi huku wakiangua vilio, wakijipiga vifua na kuomboleza kifo cha kiongozi wao na kutoa heshima zao za mwisho.

Mrithi wa kiongozi huyo, mwanawe wa mwisho wa kiume, Kim Jong Un, aliusindikiza mwili wa baba yake akiandamana na maafisa wakuu wa jeshi na wanachama wa chama cha tawala, akiwemo mjomba wake, Jang Song Taek.

Wachambzi wanasema Taek, ambaye alionekana kuwa naibu wa marehemu Kim Jong Ill, atamsaidia mpwa wake, Kim Jong Un, ambaye ana umri wa miaka 27, kuliongoza taifa hilo kwani hana ujuzi wa kutosha kuendesha masuala ya kitaifa kutokana na umri wake mchanga.

Wanajeshi walipiga saluti za heshima na kufyatua mizinga 21 kumuaga kiongozi wao, wakati msafara wa magari uliokuwa umebeba jeneza lake na kuongozwa na gari lililokuwa limebeba bango kubwa la picha ya marehemu likipita kuelekea katikati mwa mji mkuu, Pyongyang.

Gari lililobeba mwili wa Kim Jong Ill likipita katika mitaa ya mji mkuu wa Korea Kaskazini, Pyongyang.
Gari lililobeba mwili wa Kim Jong Ill likipita katika mitaa ya mji mkuu wa Korea Kaskazini, Pyongyang.Picha: AP

Kim Jong Ill alifariki tarehe 17 Disemba baada ya kupata mshutuko wa moyo, akiwa na umri wa miaka 69. Ameliongoza taifa hilo la Korea Kaskazini, ambalo linaegemea nadharia za kikomunisti na usiri mkubwa, kwa miaka 17. Shirika la habari la Korean Central News limesema muda rasmi wa maombelezo unatarajiwa kukamilika hapo kesho kwa misa ya wafu na dakika tatu za kuwa kimya kote nchini humo mwendo wa sita mchana.

Kim Jong Il aliongoza taifa hilo, ambalo limerodheshwa kuwa mojawapo ya mataifa maskini zaidi ulimwenguni, akitumia kikosi kikubwa sana cha kijeshi kutawala. Alitilia mkazo sana umiliki wa silaha za nyuklia, huku nchi yake ikiselelea kwenye ufukara. Inakadiriwa kuwa maelfu ya Wakorea walikufa kutokana na njaa wakati wa utawala wake.

Lakini shirika la habari la nchi hiyo limemsifu kwa kujenga msingi bora wa siku za usoni kwa taifa. Mrithi wake, Kim Jong Un, anatarajiwa kuendeleza utawala wa urithi ambao umekuwepo kwa miongo mingi katika taifa hilo kwa vizazi vitatu sasa tangu wakati wa babu yake, Kim Ill Sung.

Baada ya msafara huo kuzunguka mji huo, mwili wa marehemu umerejeshwa katika kasri ambapo utakaushwa na kuhifadhiwa.

Mwandishi: Caro Robi/DPA
Mhariri: Othman Miraji