1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kimbunga chaua 91 Oklahoma

Admin.WagnerD21 Mei 2013

Kimbunga kikubwa kilichoukumba mji wa Oklahoma nchini Marekani kimeuwa watu 91 wakiwemo watoto 20. Maafa makubwa yametokea katika kitongoji cha Moore, ambacho kimepitiwa na upepo unaosafiri kwa kasi ya Km 300 kwa saa.

https://p.dw.com/p/18bKO
Kimbunga Oklahoma
Kimbunga OklahomaPicha: Reuters

Rais wa Marekani Barrack Obama ameitangaza Oklahoma kuwa eneo la janga kubwa na kuagiza usaidizi zaidi kupelekwa katika eneo lililoathirika zaidi katika kitongoji cha Moore. Kimbunga hicho ndicho kikubwa zaidi kuikumba Marekani baada ya kile kilicholikumba eneo la Jouplin katika jimbo la Missouri miaka miwili iliyopita ambacho kiliuwa watu 166.

Maafisa wa uokozi wamekuwa wakitafuta manusura zaidi chini ya vifusi vya shule iliyoporomoka ya Plaza Towers ambayo imeathiriwa zaidi na kimbunga hicho.

Shule nyingine ya msingi ya Briarwood ,nyumba kadhaa na hospitali ni miongoni mwa majengo yaliyoangushwa na kuwaacha wakaazi wa mji huo wapatao 50,000 wakiwa wamegutushwa na janga hilo lililowaacha na msiba.

Maafa yaliyosababishwa na kimbunga Oklahoma
Maafa yaliyosababishwa na kimbunga OklahomaPicha: Reuters

Afisa wa afya wa Oklahoma amesema 20 kati ya watu 91 waliopoteza maisha yao ni watoto.Afisi ya afya ya eneo hilo imethibitisha vifo hivyo na kuongeza kuwa idadi ya waathiriwa inatarajiwa kuongezeka.

Kimbunga chauharibu sana mji wa Moore

Kati ya watu 240 waliojeruhiwa,60 kati yao ni watoto.Mtaa wa Moore umeharibiwa vibaya huku kukishuhudiwa uharibifu mkubwa wa mali na miundo mbinu na magari yaliyoharibiwa yakiwa yamerundikana.

Gavana wa jimbo hilo la Oklahoma Mary Fallin amesema leo ni siku ya huzuni kwa wakaazi wa eneo hilo.

Huku waokoaji wakiwa bado wanaendelea kutafuta manusura, taasisi za tahadhari ya vimbunga zinaonya kuwa majimbo mengine huenda pia yakakumbwa na kimbunga hicho, likiwemo Texas na mengine yaliyo kusini mwa nchi hiyo.

Kimbunga Marekani
Kimbunga MarekaniPicha: Reuters

Shirika la kitaifa la utabiri wa hali ya hewa limeorodhesha kimbunga hicho kwa kiwango cha EF4 kwenye kipimo cha Fujita hii ikimaanisha kuwa kiko katika daraja la pili la vimbunga vikali vinavyoandamana na upepo  unaovuma kwa kasi ya kilomita 320 kwa saa.

Ilani yatolewa muda mfupi kabla ya kimbunga kufika

Kituo cha kutabiri vimbunga kilitoa ilani ya mji huo wa Oklahoma kukumbwa na kimbunga dakika 16 kabla kimbunga hicho kuharibu mji huo.Mkaazi mmoja wa eneo hilo anasema muda huo ulikuwa mfupi kwa wao kukimbilia maeneo salama.

Shirika la kusimamia viwanja vya ndege limeahirisha kwa muda usafiri wa ndege katika eneo hilo na kuruhusu tu zile zinazobeba misaada kwa ajili ya waathiriwa wa eneo hilo.

Huu ni msimu wa vimbunga na vimbunga zaidi vimetabiriwa.Jumapili iliyopita vimbunga viliwauawa watu wawili na kuwajeruhi wengine 39 mjini Oklahoma.

Kulingana na maelezo ya walioshuhudia kimbunga cha usiku wa kuamkia leo,kimbunga hicho kilikuwa kikali kushinda cha mwaka 1999 ambacho kinadiriwa kuwa cha tatu kibaya zaidi katika historia ya Marekani kwani kiliharibu mali inayokisiwa kufikia dola bilioni 1 wakati huo.Vimbunga vya Joplin na Tuscaloosa vilivokumba Marekani mwaka 2011 vinaorodheshwa pia kuwa viliiletea nchi hiyo hasara kubwa.

Mwandishi: Caro Robi/Afp /dpa/Reuters

Mhariri: Daniel Gakuba.