1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kimbunga Ian chapiga Cuba

28 Septemba 2022

Kimbunga Ian kinatarajiwa kulipiga jimbo la Florida nchini Marekani, huku watabiri wa hali ya hewa wakionya juu ya dhoruba kubwa inayotishia maisha.

https://p.dw.com/p/4HSRk
Florida | Hurrikan Ian
Picha: NOAA/AP/picture alliance

Kutokana na kimbunga hicho ambacho kimewaua watu wawili huko Cuba na kulitumbukiza taifa hilo gizani kutokana na uharibifu kwenye mfumo wa gridi ya taifa.

somaKimbunga chauwa zaidi ya watu 70 Marekani

Maafisa wa huduma ya dharura wametoa maagizo ya lazima kwa wakaazi katika kaunti kadhaa za pwani ya Florida kuhama kufikia saa nane usiku saa za eneo hilo na kupendekeza watu kwenye maeneo mengine jirani kuhama kwa hiyari.

soma Kimbunga Ida chapungua kasi Marekani

Kituo cha Kitaifa cha kukabiliana na Vimbunga cha Marekani katika ushauri wake kimesema kinatarajia dhoruba hiyo kuimarika hadi itakapotoweka.

Kituo hicho cha Marekani kimedokeza kwamba kimbunga Ian kinatabiriwa kupiga katikati mwa Florida Jumatano usiku na Alhamisi asubuhi na kuelekea magharibi mwa Atlantiki kufikia Alhamisi huku wakiitaja dhoruba hiyo kama "kimbunga kikubwa na hatari sana."

Mafuriko makubwa yanatarajiwa katika sehemu za Florida ya kati, kusini, kaskazini, kusini mashariki mwa Georgia na pwani ya kusini mwa Carolina. Kimbunga hicho kitawasili Florida baada ya kuipiga Cuba.

Giza totoro

BG Kuba
Picha: ALEXANDRE MENEGHINI/REUTERS

Taasisi ya hali ya hewa ya Insmet imesema kimbuka Ian kimevuruga upatikanaji wa huduma za umeme na kuiweka Cuba gizani siku ya Jumanne baada ya kupiga magharibi mwa nchi hiyo kwa zaidi ya saa tano kabla ya kupiga tena kwenye Ghuba ya Mexico.

Mkurugenzi wa kiufundi wa mfumo wa Umeme wa Cuba (UNE) Lazaro Guerra alisema mfumo huo ulikuwa na matatizo kutokana na kimbunga hicho.

Guerra amesema "Kwa sasa, mfumo wa umeme unapitia hali tete. Mfumo umeharibika kabisa, hii inamaanisha kuwa hakuna huduma ya umeme nchini kote. Mfumo tayari ulikuwa chini ya shinikizo. Tulikuwa na eneo kubwa katika sehemu ya magharibi ya nchi bila huduma yoyote, ikiwa ni pamoja na Havana ambayo ni sehemu muhimu ya huduma za umeme."

Ni watu wachache tu waliokuwa na jenereta zinazotumia petroli walioweza kupata umeme kwenye kisiwa hicho chenye zaidi ya watu milioni 11. Wengine walilazimika kufanya kazi na tochi au mishumaa nyumbani, na kutumia mwangaza wa simu za rununu walipokuwa wakitembea mitaani.

Katika mji wa magharibi wa Pinar del Rio, video za shirika la habari la AFP zilionyesha nyaya za umeme zilizoanguka, mitaa iliyofurika maji na kutawanyika kwa paa zilizoharibika.

Kwa mujibu wa Mamlaka za mji huo takriban watu 40,000 walihamishwa baada ya kukabiliwa na madhara makubwa zaidi ya dhoruba hiyo.

/AP/AFP