1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kimbunga Irma chaendelea kupiga Florida

Josephat Charo
11 Septemba 2017

Kimbunga Irma kimeendelea kupiga jimbo la Florida nchini Marekani kikiangusha winchi, kuharibu barabara na kuwaacha mamilioni ya watu bila umeme.

https://p.dw.com/p/2jhQl
USA Florida Hurrikan Irma
Picha: Reuters/S. Yang

Kimbunga hicho kikali kimepiga kwa mara ya pili katika kisiwa cha Marco huku kikiandamana na upepo unaovuma kwa kasi ya kilomita 209 kwa saa, kwa mujibu wa kituo cha kitaifa kinachofuatilia vimbunga.

Wakazi milioni sita wa jimbo la Florida waliamriwa waondoke katika zoezi kubwa kabisa la kuwahamisha watu katika maeneo salama katika historia ya Marekani.  Winchi mbili kubwa za ujenzi ziliangushwa na upepo mkali ulioandamana na kimbunga hicho mjini Miami.

Rais wa Marekani Donald Trump ameridhia ombi la jimbo la Florida kutaka msaada wa dharura wa fedha wa kusaidia juhudi za kuondokana na athari za kimbunga Irma. Trump amesema atakwenda Florida hivi karibuni kuangalia jinsi juhudi za uokoaji na utoaji misaada zinavyoendelea.

"Nadhani kazi inaendelea vizuri. Walinzi wa pwani wamekuwa wakichapa kazi kwa bidii. Tunashirikiana vizuri na gavana wa Florida na magava wa majimbo jirani. Baraza lote la mawaziri limejitokeza na kila kundi linaratibiwa vizuri. Taarifa mbaya ni kwamba kimbunga hiki ni kikubwa mno na kibaya, lakini nadhani tunashirikiana na tumejipanga vyema kabisa."

Muda mfupi baada ya kupiga kisiwa cha Marco, nguvu ya kimbunga hicho ilipungua na hivyo kuorodheshwa kuwa katika kiwango cha pili cha hatari wakati kilipopiga mji wa Neaples, mji maarufu kwa watalii. Watabiri wa hali ya hewa wameonya bado kimbunga hicho ni hatari, huku kima cha maji kikifikia hadi mita 2.1 chini ya kipindi cha masaa mawili.

USA Florida Hurrikan Irma
Winchi iliyoangushwa na upepo mkali MiamiPicha: Reuters/C. Barria

Mkurugenzi anayesimamia utoaji wa huduma za dharura Florida Bryan Koon anasema hajafaulu kutathmini uharibifu uliosababishwa na kimbunga Irma. Koon amesema angalau uwanja mmoja wa ndege wa Keys unafanya kazi na anatumai wafanyakazi kazi wa kutoa misaada wataweza kusafiri kwa ndege kujionea uharibifu uliosababishwa na zilzala hiyo.

"Hali ya hewa imekuwa mbaya sana mchana kutwa kiasi cha kutoweza kusafiri kwa ndege. Hatuna taarifa kamili kuhusu uharibifu uliosababishwa na kimbunga Irma. Sina takwimu zozote za watu ambao huenda wamejeruhiwa. Tutashughulikia suala hilo kesho kukipambazuka."

Athari kubwa zajitokeza

Zaidi ya watu milioni nne waliachwa bila umeme kwa mujibu wa kitengo cha huduma za dharura cha Florida. Kampuni ya umeme ya Florida imesema imefaulu kuvifunga vinu viwili vya nyuklia katika mtambo wake wa kufua umeme.

USA Hurrikan Irma in Miami
Watu wakiwa katika kituo cha hifadhiPicha: picture-alliance/ZUMA Wire/Xinhua/Y. Bogu

Mahema katika mji wa Tampa, Florida yamefurika watu huku kimbunga Irma kikipinda kuelekea upande wa magharibi na kikitarajiwa kupita maeneo yaliyojaa watu ambayo hayajajiandaa eneo la magharibi la jimbo hilo. Kufikia jana njia zote za kukimbilia zilifungwa kwa watu waliotaka kuondoka Florida. Hata hivyo wakaazi wa eneo la magharibi walibaki kwa sababu kubadilika ghafla kwa mkondo wa kimbunga hicho, kulitokea bila wao kutarajia na hawakuwa na chaguo lengine bali kukimbilia katika maeneo maalumu ya hifadhi yaliyotayarishwa kujistiri.

Katika shule moja inayotumiwa kama makazi ya muda, watu zaidi ya 2,000 wameonekana ndani ya kituo hicho kinachoweza kuwahifadhi mamia ya kadhaa ya watu. Wengine waliamua kurejea makwao badala ya kukaa mahala hapo paolipofurika watu.

Catherine, msimamizi wa kituo hicho, anasema licha ya uhaba wa mahitaji muhimu, hawawezi kuwafungia nje watu wanaotaka kuingia.

"Bila shaka tutaomba msaada wa chakula zaidi. Tutaomba kila kitu tunachokihitaji. Bila shaka chakula kingi kwa ababu hatutaweza kupeleka malori ya vyakula na bidhaa nyeingine mpka upepo mkali utakapotulia tena. Siwezi kutabiri lini hilo litakapotokea."

Kimbunga Irma kiliua mtu mmoja Marekani, mwanamume aliyepatikana amekufa katika gari aina ya pick up ambayo ilikuwa imegonga mti katika mji wa Marathon huko Florida Keys. Kimbunga hicho kiliwaua watu wapatao 28 kilipoelekea upande wa magharibi kikipitia eneo la Karibik kuelekea Florida na kusababisah uharibifu katika visiwa kadhaa vidogo na Puerto Rico, Jamhuri ya Dominican na Haiti kabla kupiga maeneo ya kaskazini mwa Cuba.

Mwandishi:Josephat Charo /afpe/rtre

Mhariri:Iddi Sessanga