1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Kinachohitajika sasa ni badiliko katika fikra"

Maja Dreyer6 Desemba 2007

Wakati wataalamu kutoka kila pembe ya dunia wanaendelea mkutano wao huko Bali, Indonesia, unaolenga kupunguza utoaji wa gesi chafu na hivyo kusimamisha ongezeko la ujoto ulimwenguni, Ujerumani pia imeongeza juhudi zake.

https://p.dw.com/p/CYSq
Ujerumani inataka kuongeza matumizi ya nishati endelevuPicha: AP

Jana serikali ya Ujerumani ilipitisha mradi mkubwa wenye kutoa motisha kutumia nishati endelevu na kupunguza matumizi ya nishati. Waziri wa mazingira wa Ujerumani, Sigmar Gabriel, alisifu mradi huu kama mafanikio makubwa, lakini wahariri wa magazeti yaliyochapishwa leo humu nchini wana maoni tofauti. Tusikie basi kwanza uchambuzi wa gazeti la “Neues Deutschland”. Limeandika:


“Kweli hatukuamini kuwa serikali hiyo ya mseto itaweza kupitisha mradi mkubwa wa kutunza hali ya hewa. Kwa ujumla, sheria 14 zinatakiwa kurekebishwa ili Ujerumani iweze kupunguza utoaji wa gesi ya Carbon Dioxide kwa asilimia 40 hadi mwaka wa 2020. Hata hivyo, lengo hili halitaweza kufikiwa kupitia hatua zilizoamuliwa. Mfano sekta ya usafiri ambayo inatoa gesi nyingi haihusishwi.”


Ni maoni ya mhariri wa gazeti la “Neues Deutschland”. Mwenzake wa “Rhein-Neckar-Zeitung” anakubali naye akisema kwamba haijulikani ikiwa kiwango cha kupunguza utoaji wa gesi ya Carbon Dioxide kitaweza kufikiwa, hata hivyo anasisitiza kwamba:


“Ingekuwa kosa kubwa kupuuza hatua hiyo ya kuingia katika enzi mpya ya sera za nishati endelevu. Kinachohitajika sasa ni badiliko katika fikra kwani hadi sasa tuliamini ukuaji wa uchumi na ustawi wa umma utapatikana tu kwa kutumia nishati nyingi.”

Gazeti la “Hamburger Abendblatt” linaonya kutokuwa na matarajio mengi juu ya mradi huu mpya wa serikali:


“Yule ambaye tayari ana friji ambayo bado inafanya kazi hatanunua friji mpya ambayo inatumia nishati ndogo tu. Na wananchi wakilazimishwa kulipa gharama kubwa zaidi kwa umeme kwa sababu umeme sasa umetengenezwa kwa njia endelevu, hata hivyo watakasirika. Kwa hiyo, mradi huu wa Ujerumani kutunza mazingira utachukua muda mrefu kuleta matokeo.”


Naam, na hatimaye tuyasikie maoni ya mhariri wa “Ostthüringer Zeitung” ambaye anaangalia siku za usoni:

“Bado ni siri vipi Kansela Angela Merkel anayejionyesha kama mwanaharakati wa mazingira ataweza kufikia lengo lake la kupunguza utoaji wa gesi ya Carbon Dioxide kwa kiwango hiki kikubwa. Kujenga mitambo mingine ya kutengeneza nishati endelevu au kupunguza matumizi ya nishati ni hatua ambazo peke yake hazitatosha. Huenda mikutano kama ule wa Bali nchini Indonesia unaoendelea hivi sasa inatoa picha kama hii. Lakini kwa kufanya hivi tu hatutaweza kuzuia barafu kuyeyuka au dubu anayeishi kwenye barafu kuangamizwa. Badala yake inabidi wataalamu na wahandisi wote wa dunia wakusanye ujuzi wao.”