1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KINSHASA :Mapigano yameibuka mashariki mwa Kongo

26 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCp9

Duru za kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo zinasema,mapigano yameibuka upya katika mji wa Sake kati ya majeshi ya serikali na vikosi vinavyomtii Laurent Nkunda alieasi.Kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa,vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa pia vilipambana na waasi baada ya majeshi ya serikali kuukimbia mji huo.Siku ya Jumamosi,vituo vya kijeshi vilishambuliwa na vikosi vinavyomuunga mkono Nkunda.Wanajeshi 2 wa serikali waliuawa na vile vile raia kwa maelfu wameuhama mji kwa sababu ya mapigano hayo.Hali ya machafuko inaendelea katika maeneo ya mashariki nchini Kongo,licha ya kuwepo kwa vikosi vya Umoja wa Mataifa na makubaliano ya amani ya mwaka 2003.Rasmi,mkataba huo wa amani umemaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka mitano.Zaidi ya wanajeshi 17,000 wa Umoja wa Mataifa wanasimamia amani katika eneo hilo.