1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KINSHASHA : Wanajeshi washtakiwa kwa uhalifu wa vita

28 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCfm

Kundi la wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wamefikishwa mahkamani kwa mashtaka ya uhalifu wa vita hapo jana ikiwa ni mwezi mmoja baada ya wachunguzi wa Umoja wa Mataifa kugunduwa makaburi ya pamoja ndani ya kambi moja ya kijeshi yakiwa na maiti 30 zikiwemo za wanawake na watoto.

Washtakiwa hao 14 walikuwa wako kwenye kambi ya Bavi ilioko kilomita 40 kusini mwa Bunia mji mkuu wa wilaya Ituri.

Timu ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa imegunduwa maiti hizo mwishoni mwa mwezi wa Novema katika makaburi matatu ya pamoja ambayo yalionekana kwamba yalifukiwa hivi karibuni.

Kesi hiyo inaendeshwa na mahkama ya kijeshi huko Bunia na iwapo washtakiwa watapatikana na hatia wanaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

Umoja wa Mataifa unaamini kwamba wahanga wa mauaji hayo walitoweka wakati wa operesheni za kijeshi dhidi ya wanamgambo wa kienyeji mwishoni mwa mwezi wa Augusti na mapema mwezi wa Septemba kuelekea marudio ya uchaguzi wa urais wa mwezi wa Oktoba.