1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kinyang'anyiro Baraza la Usalama chaingia hatua ya mwisho

Thelma Mwadzaya12 Oktoba 2010

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linapiga kura baadaye leo kuzichagua nchi tano kuingia kwenye Baraza la Usalama la Umoja huo. Ujerumani ni miongoni mwa nchi zinazowania kiti kwenye Baraza hilo

https://p.dw.com/p/PcuZ

Uchaguzi wa mara hii unafanyika kwa msisimko wa aina yake. Canada, Ujerumani na Ureno zinapigania viti viwili ambavyo vitawachwa wazi na Uturuki na Austria, ifikapo mwishoni kabisa mwa mwaka huu. Huu utakuwa ni ushindani mzito, kwa kuwa wagombea ni watatu na nafasi ni mbili. Kazi kubwa ya kampeni imekuwa ikiendeshwa miongoni mwa wajumbe wa mataifa 192 ya Umoja wa Mataifa.

Lakini kwa Afrika ya Kusini, India na Colombia hakuna mapambano makubwa. Nafasi wanazogombea hazina washindani. Mataifa haya yatachukua nafasi za Uganda, Japan na Mexico ambayo nayo yanamaliza muhula wao mwishoni mwa mwaka. Hata hivyo, ili nchi iweze kupata kiti katika Baraza hili, lazima ipate robo tatu ya kura 192 za Mkutano Mkuu wa Umoja huo.

Kawaida wagombeaji huchaguliwa na nchi kutoka kila eneo miongoni mwa maeneo matatu ya dunia ili kuepusha ushindani usiokuwa na ulazima. Lakini kwa kuwa mara hii kundi la Ulaya Magharibi, linalozijumuisha pia Israel, Australia na New Zealand halikuweza kukubaliana juu ya nchi mbili zinazofaa kuchukua nafasi zitakazowachwa wazi na Uturuki na Austria, ndio maana pana wagombea watatu kwa nafasi mbili.

Lakini, licha ya ushindani huo, Balozi wa Ujerumani nchini Marekani, Jürgen Chrobog, anadhani kwamba hivi sasa ni muhimu kuliko wakati wowote huko nyuma kwa Ujerumani kuwa na kiti kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

"Naamini kwamba si lazima sisi tuwe lakini hili ni jambo muhimu kwetu. Na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, ameweka wazi msimamo huo. Tunataka tupewe dhamana hii, maana tayari tunachukuwa dhamana nyengine nyingi tu za Umoja wa Mataifa. Tumekuwa ni sehemu ya karibu kila ujumbe wa amani wa Umoja huu. Tuna karibuni wanajeshi wetu 6,300 wanaohudumu kwenye maeneo yenye migogoro duniani. Tunadhani kwamba wakati umefika wa sisi pia kuwa sehemu ya wale wanaoweza kufanya maamuzi kwenye Baraza la Usalama." Anasema Bwana Chrobog.

Baraza la Usalama linaundwa na wajumbe 15, ambapo watano kati yao ni wa kudumu na kumi huchaguliwa kwa vipindi vya miaka miwili miwili. Wajumbe wa kudumu na Marekani, Urusi, Ufaransa, China na Uingereza. Wajumbe hawa wana kura ya turufu juu ya maamuzi yoyote ya Umoja wa Mataifa na, kwa hivyo, wana ushawishi mkubwa katika mchakato mzima wa kufikiwa maamuzi hayo.

Wanadiplomasia wanasema kwamba, kinachofanya uchaguzi wa leo uwe na hamasa ni kwamba, uwezekano wa kuwemo kwa timu ya mataifa matano, ambayo yana uchumi na ushawishi katika maeneo yao, kwenye Baraza la Usalama la mwaka 2011, kutalipa taswira mpya Baraza hilo. Mataifa hayo ni Afrika ya Kusini, Nigeria, India, Brazil na huenda pia Ujerumani.

Hivi sasa, pamoja na kugombea ujumbe huu wa miaka miwili, mataifa haya tayari yameshasema kwamba yanataka ujumbe wa kudumu kwenye Baraza hili, wito ambao unahitaji marekebisho makubwa katika sheria na taratibu za Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo, wakosoaji wanasema kwamba siasa za uhafidhina na kutumiliana zilizomo kwenye Umoja huu zinaweza kukwamisha azma hii ya wanamageuzi kwenye Umoja huo. Mijadala ya kulibadilisha na kuliongeza Baraza la Usalama ilianza kuletwa kwenye mikutano ya umoja huo tangu kwenye miaka ya 1980, ambapo ilipendekezwa wajumbe wa Baraza wawe 21 au 26 badala ya 15 wa sasa ili kuakisi matakwa ya wanachama wa Umoja huo.

Lakini kitu pekee kilichoweza kufikiwa kwenye mijadala hiyo ni kulifanya Baraza la Usalama kuwa na uwazi zaidi, na sio kulibadilisha Baraza lenyewe.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPAE

Mhariri: Josephat Charo