1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi mpya wa kanisa katoliki aapishwa

19 Machi 2013

Waumini wasiopungua milioni moja wamemshangiria Papa Francis wa kwanza alipowasili katika uwanja wa Mtakatifu Petrus kwa misa ya kumkabidhi wadhifa wake,wakitaraji kanisa litakuwa karibu zaidi na waumini.

https://p.dw.com/p/1801h
Papa Francis katika ibada ya kuapishwaPicha: picture-alliance/dpa

Akivalia joho jeupe na skola ya rangi hiyo hiyo huku akitabasamu,Papa huyo wa kwanza wa kutoka bara la Amerika aliingia katika uwanja wa Mtakatifu Petrus akiwa ndani ya gari lisilokuwa na paa,akishangiriwa kwa matarumbeta na shangwe za malaki ya waumini.Bendera za ulimwengu mzima zinapepea katika uwanja huo unaong'ara kwa kijua cha msimu wa machipuko.

Baada ya kuuzunguka uwanja wa mtakatifu Petrus Papa Francis wa kwanza akifuatana na makadinali,wakiwemo wale wa kanisa la kikatoliki la Mashriki,alikwenda kusali katika kanisa la muasisi wa kanisa katoliki

"Ni tukio linaloanzisha mtazamo mpya wa kanisa-pamoja na Papa Francis wa kwanza tutakuwa na kanisa lililo karibu zaidi na umma na ulimwrngu wa kimambo leo" amesema hayo muumini mmoja kijana anaetokea Colombia.

Papa Francis wa kwanza aliyeachana na mtindo wa kupanda gari la viyoo vya kinga,alisimamisha kwa muda gari yake na kuteremka ili kumbariki bwana mmoja mlemavu.

Jukumu la Papa ni unyenyekevu

Papst Franziskus Amtseinführung
Papa Francis wa kwanza aapishwa katika uwanja wa Mtakatifu Petrus mjini RomaPicha: Reuters

Zaidi ya tume 130 kutoka nchi za nje,wafalme sita,viongozi zaidi ya 30 wa taifa na serikali akiwemo kansela Angela Merkel na makamo wa rais wa Marekani Joe Biden na viongozi wa kidini wamewasili katika uwanja wa mtakatifu Petrus mjini Roma wakitokea katika kila pembe ya dunia.Wawakilishi wa dini ya kiyahudi na kiislam na wale wa kiorthodox wanahudhuria pia misa hiyo ya kuapishwa Papa Francis wa kwanza.

Baada ya kuvikwa skola na pete kuashiria sasa amekuwa kiongozi wa 266 wa kanisa katoliki ulimwenguni,Papa Francis wa kwanza alisema "madaraka ya kweli ya Papa ni "huduma za dhati na unyenyekevu".Papa Francis wa kwanza amesema Papa anabidi anyoshe mikono yake kwa ulimwengu mzima na hasa kwa wanyonge,watu walio masikini na dhaifu."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Mohammed Abdul-rahman