1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani: Ina taarifa juu ya mauaji ya Abu Firas al-Suri

Mjahida 4 Aprili 2016

Msemaji wa kundi linalofungamanishwa na kundi la al Qaeda, Al Nusra Front ameuwawa pamoja na mtoto wake wa kiume na wapiganaji wengine 20 wa jihadi, katika mashambulio ya angani Kaskazini Mashariki mwa Syria.

https://p.dw.com/p/1IOyS
Syrien IS Al-Nusra Front Kämpfer
Wanachama wa kundi la Al Nusra FrontPicha: picture alliance/ZUMA Press/M. Dairieh

Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la uangalizi wa haki za binaadamu nchini Syria, Rami Abdel Rahman, Abu Firas al-Suri alikuwa anakutana na wapiganaji wengine waliyo na itikadi kali, katika ngome ya Kafar Jales ya kundi la al Nusra Front wakati waliposhambuliwa.

Hata hivyo bado haijawa wazi iwapo mashambulizi hayo ya angani yalifanywa na ndege za kivita za kutoka serikali ya Syria au mshirika wake wa karibu Urusi.

Abu Firas al-Suri ambaye jina lake halisi ni Radwan Nammous, alipigana dhidi ya vikosi vya kisovieti nchini Afghanistan ambako alikutana na kiongozi wa Al Qaeda Osama bin Laden pamoja na mshauri wake Abdullah Azzam kabla ya kurejea nchini Syria mwaka wa 2011.

IS Fahne Syrien Nusra Front
Kundi la Al Nusra FrontPicha: picture-alliance/AP Photo/Malla

Marekani iliyokuwa ikipambana na kundi la Al Nusra Front kwa muda mrefu imesema inataarifa juu ya kuuwawa kwa Al Suri lakini haikuwa na taarifa zaidi za kutoa juu ya kifo chake.

Kando na hayo maeneo mengine yanayoshikiliwa na kundi hilo la Al Nusra Front na kundi jengine linaloshirikiana nalo la Jund al-Aqsa, Kaskazini mwa mji wa Idlib pia yalishambuliwa na kuwajeruhi wengi.

Mazungumzo juu ya hatima ya Assad huenda yakazuwiya upatikanaji wa suluhu la kisiasa.

Wakati huo huo makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano yaliyokubaliwa kati ya vikosi vya serikali na waasi yameendelea kuheshimiwa tangu tarehe 27 mwezi wa Februari, lakini makubaliano hayo hayawajumuishi makundi ya Al Nusra Front na kundi la wanamgambo wa dola la kiislamu.

Syrien Russland Treffen Baschar al-Assad Sergej Rjabkow
Rais wa Syria Bashar al Assad, na Naibu Waziri wa Mambo ya nje wa Urusi Sergei RyabkovPicha: Reuters

Makubaliano hayo yameipa nafasi Urusi na muungano unaoongozwa na Marekani waliokuwa wanalishambulia kundi la IS nchini Syria, kuunganisha nguvu zao dhidi ya makundi ya jihadi.

Huku hayo yakiarifiwa shinikizo la kumtaka rais wa Syria Bashar al Assad kungatuka madarakani huenda ikazuwiya upatikanaji wa suluhu la kisiasa nchini humo, hii ni kwa mujibu wa shirika la habari la Urusi RIA lililomnukuu Naibu Waziri wa nchi za nje wa Urusi Sergei Ryabkov. Moscow imependekeza mazungumzo juu ya hatima ya Assad yasimamishwe huku ikisema suala hilo linapaswa kujadiliwa na kuamuliwa baadaye na pande husika katika mgogoro wa Syria.

Mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa miaka mitano Syria yamesababisha mauaji ya watu zaidi ya 270,000 huku mamilioni ya wengine wakiachwa bila makao na kundi kubwa likikimbilia barani Ulaya.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP

Mhariri: Yusuf Saumu