1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa al-Qaeda nchini Yemen al-Awlaki auwawa

1 Oktoba 2011

Mhubiri wa dini ya Kiislamu mzaliwa wa Marekani na mtu maarufu katika kundi la al-Qaeda Anwar al-Awlaki , ameuwawa katika shambulio la anga la Marekani mashariki ya Yemen.

https://p.dw.com/p/12kBJ
Imam Anwar al-Awlaki mzaliwa na raia wa Marekani akiwa nchini Yemen.Picha: dapd

Mhubiri wa dini ya Kiislamu mzaliwa wa Marekani na mtu maarufu katika kundi la al-Qaeda, ameuwawa katika shambulio la Marekani mashariki ya Yemen. Anwar al-Awlaki mara nyingi alitoa hotuba kwa lugha ya Kiingereza kutoka Yemen akihimiza mashambulizi dhidi ya Marekani na alikuwa raia wa kwanza wa Marekani kuwekwa katika orodha ya shirika la ujasusi la Marekani ya kukamatwa ama kuuawa.

Rais Barack Obama amesema, maelezo yake yenye chuki yamehusika na mashambulizi ya hapo zamani dhidi ya Marekani. Hata hivyo , mashirika ya haki za kijamii yametaka kujua uhalali wa kumlenga raia wa Marekani ambae hajashtakiwa mahakamani kwa uhalifu. Chama cha umoja wa haki za kiraia nchini Marekani kimesema, kuuawa kwa Awlaki kunaonyesha kuwa raia wa Marekani huenda wakauawa na serikali yao bila kufikishwa mahakamani.