1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa Irak azuru nchi isiyo pendelewa na Marekani

20 Agosti 2007

Waziri mkuu wa Irak Nouri al Malik ameanza ziara yake nchini Syria huku mauaji yakiendelea nchini mwake.

https://p.dw.com/p/CH9P
Nouri al-Malik waziri mkuu wa Irak
Nouri al-Malik waziri mkuu wa IrakPicha: AP

Nouri al Malik ni waziri mkuu wa kwanza wa Irak kuwahi kuzuru Syria tangu Marekani ilipoivamia Baghdad na kumng’oa madarakani Saddam Hussein mwaka 2003 na kusababisha hali ya ukosefu wa usalama nchini humo uliozusha wimbi la wakimbizi zaidi ya milioni moja kukimbilia nchini Syria.

Bila shaka ziara ya waziri mkuu wa Irak itazingatia mengi kuhusu hali ya usalama pamoja na kuishawishi serikali ya rais Bashar al Assad ichukuwe hatua ya kuzuia wimbi la wapiganaji wenye msimamo mkali na pia uingizaji wa silaha nchini Irak kupitia mpakani kati ya Syria na Irak.

Msemaji wa serikali ya Irak Ali al-Dabbagh amesema kwamba mazungumzo baina ya viongozi wa nchi hizo mbili pia yatagusia hali ya uchumi na uhusiano kati ya nchi hizo.

Nouri al- Malik aliishi uhamishoni nchini Syria kwa miaka kadhaa akiwa mwanachama wa upinzani wakati wa utawala wa Saddam Hussein.

Waziri mkuu wa Irak Nouri al Maliki tayari amekutana na mwenziwe wa Syria Naji al- Qatari mjini Damascus na anatarajiwa kufanya mazungumzo na rais Bashar al Assad kesho Jumanne.

Damascus mwanzoni mwa mwezi huu ilidhamini mkutano wa kimataifa uliojadili hali ya usalama nchini Irak ambako Syria na nchi zingine jirani zilitakiwa zisaidie kuimarisha hali ya usalama nchini humo ili pia kujikinga na makundi ya wapiganaji wenye msimamo mkali ndani ya nchi zao.

Katika mkutano huo Syria ilikubali kwamba itashiriki katika mtandao wa upelelezi ili kuisaidia serikali ya Irak inayoungwa mkono na Marekani kupambana na waasi na pia kujaribu kukabiliana na uingizaji haramu wa silaha kupita maeneo ya mpakani.

Hata hivyo Irak imesema Syria bado haijaweka kasi katika ahadi hizo.

Marekani inazilaumu Syria na Iran kwa kuchochea hali mbaya ya usalama nchini Irak.

Kwa pamoja Damascus na Tehran zimekanusha madai ya Marekani na kudai kuwa usalama wa Irak ni muhimu pia kwa nchi hizo.

Ziara ya waziri mkuu Nouri al Malik nchini Syria inafutia ziara ya rais Jalal Talabani na waziri wa mambo ya ndani wa Irak nchini humo.

Huku waziri huyo mkuu wa Irak akiwa ziarani mjini Damascus takriban watu watano wameuwawa katika shambulio la bomu la kutegwa ndani ya gari katika mji wa Kishia wa Sadr kaskazini mashariki mwa Baghdad.

Mji wa Sadr ni ngome ya kikosi cha wapiganaji wa Mehdi watiifu kwa kiongozi wa kidini Moqtada al Sadr anaepinga sera za Marekani nchini Irak.

Kwengineko gavana Mohammed Al al- Hassan wa mji wa Sammawa kusini mwa mkoa wa Muthanna ameuwawa katika shambulio la bomu lililotegwa kando ya barabara alipokuwa akielekea kazini.

Huyo ni gavana wa pili kuuwawa katika kipindi cha wiki mbili.

Jeshi la Marekani limetangaza operesheni mpya ya kupambana na wapiganaji wa makundi yenye msimamo mkali kabla ya kutolewa ripoti mpya juu ya vita vya Irak inayotarajiwa kuwasilishwa mbele ya bunge la Marekani katikati ya mwezi Septemba.

Washington inahofia kwamba wapiganaji wa Al Qaeda na wa Kishia huenda wakazidisha mashambulio na kuwa chanzo au kishawishi cha majadiliano makali kuhusu vita vya Irak vinavyozidi kupoteza uungwaji mkono nchini Marekani.