1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa IS ataka wafuasi kuipigania Mosul

Isaac Gamba
3 Novemba 2016

Kiongozi wa kundi la itikadi linalojiita Dola la Kiisilamu ametoa ujumbe kupitia mkanda wa vidio akiwahamasisha wafuasi wa kundi hilo waendelee kupigana  dhidi ya vikosi vya serikali ya Iraq kuwania udhibiti wa Mosul.

https://p.dw.com/p/2S55u
Irak Militäroffensive in Mossul
Picha: picture-alliance/abaca/A. Izgi

Kwa mujibu wa kundi hilo ujumbe huo wa sauti uliorekodiwa kwa urefu wa zaidi ya nusu saa  unaoaminika kutoka kwa Abu Bakr al- Baghdadi ulisambazwa hapo jana.

Katika mkanda huo wa vidio, al Baghdadi anawataka wapiganaji wa kundi hilo hasa waloiko Mosul kupigana huku wakiendelea kuwa watiiifu kwa kundi hilo na huku pia akiwataka wapiganaji wengine wa IS kufanya mashambulizi nchini Saudi Arabia na Uturuki.

Ujumbe huo uliorekodiwa kwa njia ya sauti ni wa kwanza  kutoka kwa al-Baghdadi kwa wafuasi wa kundi hilo tangu vikosi vya Iraq vilipoanzisha operesheni ya kuukomboa kutoka mikononi mwa IS mji wa Mosul   ambao ni mji wa pili kwa ukubwa nchini humo:

Ujumbe huo unalenga kuwashawishi wasuni kuliunga mkono kundi la IS baada ya vitendo vilivyotokea mwaka 2014 wakati kundi hilo la itikadi kali lilipokamata mji huo.

Akitumia maneno yalionekana kuwa kama ya uchonganishi al Baghdad katika ujumbe wake huo alisema washia wanataka kuwaondoa wasuni katika mji huo kwa lengo la kuingiza jamii ambayo kwa maelezo yake ni watu wabaya katika mji huo.

Kiongozi huyo wa IS ametoa mwito kwa wapiganaji hao wa IS kujibu mashambulizi ya aina yoyote ile dhidi ya kundi hilo. Ujumbe huo wa sauti haukuweza kuthibitishwa mara moja  lakini unafanana na ujumbe uliowahi kutolewa hapo kabla na al- Baghdadi.

Awataka wafuasi wa kundi hilo kutojisalimisha kirahisi

Bildergalerie zum ARD Special über Abu Bakr al-Baghdadi IS Anführer
Kiongozi wa IS Abu Bakr al-BaghdadiPicha: NDR

Katika ujumbe wake huo amewataka wale wanaofikiria pengine kuyahama makazi yao kutofanya hivyo akisema ni heshima kubwa kupigana kuendelea kubaki katika eneo lako kuliko kukubali kuondolewa kirahisi.  Bado haijulikani aliko Baghdadi kwasasa ambaye ni muiraq na ambaye pia  jina lake  halisi ni Ibrahim al-Samarrai ingawa pia kuna taarifa kuwa anaweza kuwa katika mji wa Mosul au katika eneo lililo upande wa magharibi wa mji huo mpakani na  Syria  linalodhibitiwa na IS

Kundi hilo la Dola la Kiisilamu linapigana  kuendelea kuudhibiti mji wa Mosul mnamo wakati vikosi vya Iraq pamoja na wapiganaji wa kikurdi wakizidi kusonga mbele kuelekea katika mji huo kwa msaada wa muungano unaoongozwa na Marekani katika mapambano dhidi ya kundi hilo.

Mji wa Mosul wenye wakazi zaidi ya milioni moja pamoja na maeneo yake ya jirani uliangukia mikononi mwa kundi la Dola la Kiisilamu baada ya kundi hilo kufanya shambulizi la kusitukiza katika mji huo mnamo mwaka 2014.

 Baada ya kundi la IS kufanikiwa kuudhibiti mji wa Mosul Al-Baghdadi alizuru katika mji huo na kutangaza  mji huo  kuwa chini ya himaya ya Kiisilamu.

Mwandishi: Isaac Gamba/ ape/rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga