1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa ngazi ya juu wa al-Shabaab auawa Somalia

29 Oktoba 2013

Kiongozi wa ngazi ya juu anayeongoza mashambulizi ya kujitoa mhanga ya kundi la al-Shabaab lenye mafungamano na al-Qaeda ameuawa katika shambulizi la ndege isiyoruka na rubani Kusini mwa Somalia

https://p.dw.com/p/1A7eF
Picha: picture-alliance/AP

Waziri wa Mambo ya Ndani, Abdikarin Hussein Guled, ameiambia redio ya serikali kuwa idara ya ujasusi ilikuwa ikimfuatilia Ibrahim Ali Abdi, maarufu kama Anta-Anta, kwa muda sasa kabla ya shambulizi hilo kufanywa jana Jumatatu 28.10.2013

Waziri huyo hajasema ni nani aliyefanya shambulizi hilo, lakini afisa mmoja mjini Washington amesema jeshi la Marekani lilifanya shambulizi la ndege isiyoruka na rubani likililenga kundi la al-Shabaab nchini Somalia jana Jumatatu.

"Operesheni hiyo ambayo mtu huyu aliuawa ilikuwa muhimu kwa serikali. Mtu huyu alikuwa na jukumu kubwa kwa raia wengi wasio na hatia na kifo chake kitasaidia kurejesha amani," alisema waziri huyo kupitia Radio Mogadishu.

Maafisa kutoka serikali ya Somalia inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa wamemtaja mwanamgambo aliyeuawa kuwa anayefahamika vyema kwa kutengeneza mabomu ya kuvaa mwilini pamoja na ya kutengwa ndani ya gari ambayo hutumiwa mara kwa mara na waasi kuyashambulia maeneo ya serikali. Hapajakuwa na kauli yoyote kutoka kwa wapiganaji hao.

Ndege ya Marekani isiyoruka na rubani, MQ-1 Predator
Ndege ya Marekani isiyoruka na rubani, MQ-1 PredatorPicha: picture-alliance/dpa

Shambulizi hilo linakuja wiki chache baada ya shambulizi kali kufanywa katika jumba la maduka ya Westgate jijini Nairobi, Kenya, lililodaiwa kufanywa na al-Shabaab ambapo watu 67 waliuawa.

Kisha kikosi maalumu cha jeshi la wanamaji la Marekani kikafanya shambulizi katika bandari ya kusini ya Barawe mapema mwezi huu (Oktoba) na kushindwa kufikia lengo lake: ambalo lilikuwa ni kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa al-Shabaab na Mkenya mwenye asili ya kisomali kwa jina Abdulkadir Mohammed Abdulkadir, pia anayefahamika kama Ikrima.

Afisa mmoja wa Marekani ambaye hakutaka kutajwa jina lake, hajasema sehemu ambayo ndege hiyo isiyoruka na rubani ilianzia safari yake, lakini jeshi la Marekani huendesha shughuli zake za ndege hizo kutoka kambi za nchini Djibouti na Arba Minch kusini mwa Ethiopia.

Wapiganaji wa al-Shabaab wametimuliwa kutoka miji mikuu ya Somalia, ikiwa ni pamoja na Mogadishu na bandari ya kusini mwa nchi hiyo Kismayo, kufuatia operesheni ya jeshi la Umoja wa Afrika linalosimamiwa na Umoja wa Mataifa na ambalo sasa lina wanajeshi 17,700.

Kundi hilo hata hivyo linayadhibiti maeneo makubwa ya kusini mwa Somalia na katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, limekiongeza kiwango cha mashambulizi yake ya kujitoa mhanga.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Josephat Charo