1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa Taliban atangazwa kufa

Nina Markgraf7 Agosti 2009

Serikali ya Pakistan leo hii imesema inaaminika kuwa Kiongozi wa Taliban nchini humo Baitullah Mehsud ameuwawa katika shambulizi la makombora la ndege za Marekani zinazorushwa bila rubani.

https://p.dw.com/p/J5Sx
Kiongozi wa Taliban Baitullah Mehsud akizungumza na Waandishi habari Kusini mwa Waziristan mpakani mwa Afghanistan. Pakistani,May 24, 2008 akikanusha kifo chake baada ya kutangazwa wakati huo.Picha: picture-alliance/ dpa

Kifo cha Kiongozi huyo mtukukutu kitakuwa pigo kubwa katika uendeshaji wa operesheni za Taliban ambazo zilikuwa zikiongozwa nae.

Mehsud,ndie kiongozi aliyekuwa akiswakwa kwa hudi na uvumba na Marekani ambayo ilitanganza kitita cha dola milioni mia tano kwa atakaefanikisha kukamatwa kwake.

Kiongozi huyo ndiye pia amekuwa kama akitajwa kuwa kiongozi muhimu na ngazi ya juu katika kundi la mtandao wa kigaidi la Al-Qaeda.

Marekani na Pakistani zimekuwa zikimtuhumu Mehsud kwa kuwa ndiye aliyepanga mauji ya Waziri Mkuu wa Zamani wa Pakistani,Benezir Bhutto mwaka 2007.

Aidha kiongozi huyo pia ametuhumiwa kuhusika na upangaji wa mauaji ya mamia ya watu kwa kutumia mabomu kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo.

Maafisa wa ngazi za juu wa usalama wa Pakistan waliyokuwa wakisimamia Operesheni ya kumtia kizuizini Mehsud huko katika maeneo ya Waziristan wamedai mbambe huyo wa kivita ameuwawa lakini serikali ya kiraia bado inasema inaendelea kutafuta vithibitisho.

Akizungumza kupitia televisheni moja ya kibinafsi nchini humo,Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan Reheman Maliki amesema taarifa alizonazo kutoka katika eneo la tukio ni kwamba amekufa.

Waziri huyo wa Mambo ya Ndani aliongeza kuwa habari njema ni kwamba taarifa zinatoka kwa wahusika wa operesheni hiyo lakini hakuwa tayari kuthibitisha kifo hicho mpaka apate ushahidi.

Shuhuda mmoja alinukuliwa na vyombo vya habari akisema Mehsud ameuwawa akiwa na mke wake baada ya nyumba yake kuvurumishiwa makombora mawili kutoka katika ndege ya kivita isiyokuwa na rubani,huko eneo la Laddah Kusini mwa Waziristani jumatano hii.

Shirika la Ujasusi la Marekani-CIA kwa ushirikiano wa Pakistan wamekuwa wakivurumisha makombora kwa kutumia ndege zisizo na rubani na kusababisha vifo vya raia wengi bila kutaka kutao ufafanuzi wa tatizo hilo.

Marekani na Pakistan zimekuwa na jitihada za makusudi za kumuangamiza Mehsud ukiwa ni mkakati wa kupiga vita Wanamgambo wa Taliban na Mtandao wa A-Qaeda ambao wameonekana kitisho kwa Dunia na hasa katika nchi kama Pakistan ambayo ina miliki silaha za nyuklia.

Mjumbe Maalum wa Marekani nchini Pakistan Richard Holbrooke aliwambia wandishi habari mwezi uliyopita kwamba Baitullah Mehsud ni miongoni mwa watu hatari na mwenye kukasirisha wengi.

Serikali ya Pakistan imekuwa ikilalamikia mashambulio yanayofanywa na ndege za kivita zinazurushwa bila rubani pamoja na mambo mengine kwa kusema zinaharibu makazi.

Serikali hiyo nayo ilitangaza kitita cha dola za kimarekani laki sita kwa yeyote atakaefanikisha kukamatwa kwa Mehsud akiwa hai au amekufa.

Mwandishi:Sudi Mnette/AFP

Mhariri:M.Abdul-Rahman