1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa udugu wa kiislamu akamatwa Misri

Admin.WagnerD20 Agosti 2013

Maafisa nchini Misri wamesema wamemkamata Mohammed Badie huku serikali ya muda ikiimarisha juhudi zake za kukikandamiza chama cha Rais aliyeng'olewa madarakani Mohammed Mursi

https://p.dw.com/p/19SfV
Picha: picture-alliance/dpa

Kukamatwa huko kwa Mohammed Badie kumeongeza hali ya taharuki nchini Misri ambako zaidi ya watu 900 wameuawa katika siku chache zilizopita katika ghasia ambazo zimetanda kote nchini humo kati ya maafisa wa usalama na wafuasi wa Mursi

Wizara ya mambo ya ndani imesema polisi wamemkamata Badie mwenye umri wa miaka 70 karibu na uwanja wa Rabaa al Adawiya ambako zaidi ya wafuasi 200 wa Mursi waliuawa Jumatano iliyopita.

Wizara hiyo imetoa mkanda wa video unaonyesha Badie akiwa amekaa kochini na mbele yake kukiwa na chupa za maji na juisi.

Udugu wa kiislamu walengwa

Wanachama wa ngazi ya juu wa udugu wa kiislamu akiwemo Badie wameshutumiwa kwa kuchochea ghasia zilizosababisha mauaji ya mamia ya watu nchini humo kabla na baada ya kung'olewa madarakani kwa Mursi mwezi uliopita na jeshi la nchi hiyo.

Kiongozi wa udugu wa kiislamu Misri Mohammed Badie
Kiongozi wa udugu wa kiislamu Misri Mohammed BadiePicha: AFP/Getty Images

Wanachama kadhaa wa udugu wa kiislamu wamekamatwa au wanasakwa na maafisa wa usalama nchini humo.

Duru kutoka idara ya mahakama zimearifu kuwa mashitaka zaidi yamefunguliwa dhidi ya Mursi mwenyewe ambaye anazuiliwa katika eneo lisilojulikana tangu kuondolewa madarakani.

Wakati huo huo uamuzi wa mahakama hapo jana wa kumuondolea Rais wa zamani wa Misri Hosni Mubarak mashitaka matatu kati ya manne yanayomkabili yamezua uwezekano wa kiongozi huyo kuachiliwa huru.

Mahakama imeamua kuwa Muabarak anaweza kuachiliwa lakini anasalia gerezani kutokana na kesi ya nne ambayo bado inamkabili huku umwagikaji wa damu nchini humo ukiendelea baada ya wanamgambo kurusha maguruneti dhidi ya mabasi mawili yaliyokuwa yamewabeba mapolisi katika eneo la rasi ya Sinai hapo jana na kuwaua askari 25.

Rais wa zamani wa Misri Hosni Mubarak.Mahakama imemuondolea mashitaka katika kesi tatu zinazomkabili
Rais wa zamani wa Misri Hosni Mubarak.Mahakama imemuondolea mashitaka katika kesi tatu zinazomkabiliPicha: picture-alliance/dpa

Vifo vyazidi kuripotiwa Misri

Kiasi ya askari wa usalama 75 wameuawa tangu kuangushwa madarakani kwa Mursi .Shambulio hilo dhidi ya polisi linafuatia vifo vya wafungwa 37 wa udugu wa kiislamu waliokuwa wakihamishwa hadi jela iliyoko kaskazini mwa Cairo.Serikali imesema walikufa kutokana na kukosa hewa baada ya kurushwa kwa mabomu ya kutoa machozi kujaribu kumnusuru afisa wa polisi aliyekuwa ameshikwa mateka na wafungwa hao.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki Moon amesema ameshutushwa sana na vifo hivyo na kutaka uchunguzi kamili kufanywa kubaini kilichojiri haswa.

Na mwanahabari wa Misri anayefanyia gazeti la serikali Al Ahram ameuawa kwa kupigwa risasi na maafisa wa usalama na mwenzake kujeruhiwa jana jioni katika kituo cha ukaguzi cha kijeshi katika eneo la Nile Delta.

Wanahabari hao walikuwa wakirejea nyumbani baada ya mkutano na gavana wa jimbo la Beheria saa chache baada ya saa za kutotoka nje kuanza.

Jumuiya ya kimataifa imelaaani vikali ghasia za Misri huku mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International na Human rights watch yakiwataka viongozi wa Misri kusitisha mara moja agizo la kutumia risasi dhidi ya waandamanaji na kuonya kuwa nchi hiyo imetia doa rekodi yao ya kuzingatia haki za bindamu.

Umoja wa Ulaya umeitisha mkutano wa dharura hapo kesho mjini Russels kutathimini upya uhusiano wa umoja huo na Misri na msaada wa dola bilioni 6.7 unaotoa kwa nchi hiyo kila mwaka.

Mwandishi:Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Josephat Charo