1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa upinzani Livni aikosoa serikali ya Israel

22 Juni 2010

Sera mpya ya Israel kuhusu Ukanda wa Gaza, imeshambuliwa na upande wa upinzani bungeni na hata chama cha Kipalestina Hamas.

https://p.dw.com/p/NzmL
** FILE ** In this Feb. 4, 2009 file photo Israeli Foreign Minister and Kadima Party leader Tzipi Livni speaks at a campaign event in Kfar Saba, Israel. Pre-election polls show Likud Party leader Benjamin Netanyahu with a lead over Israel's Foreign Minister Tzipi Livni. Elections are scheduled for Feb. 10, 2009. (AP Photo/Tara Todras-Whitehill)
Tzipi Livni,kiongozi wa chama cha upinzani cha Kadima nchini Israel.Picha: AP

Wakati huo huo, Waziri wa Misaada ya Maendeleo wa Ujerumani, Dirk Niebel ameunga mkono hatua hiyo mpya ya Israel, kuregeza vikwazo vyake dhidi ya Gaza.

Lakini hatua hiyo ya serikali ya Israel kuregeza vikwazo vyake dhidi ya Ukanda wa Gaza imeshambuliwa na Tzipi Livni,waziri wa zamani wa mambo ya nje ambae hivi sasa ni kiongozi wa upinzani katika bunge la Israel. Livni alie pia mwenyekiti wa chama cha kiliberali cha Kadima, amemkosoa vikali Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kuwa kwa kuregeza vikwazo dhidi ya Ukanda wa Gaza, Hamas wanatambuliwa kwa hasara ya Waisraeli. Mwenyekiti huyo wa chama kikubwa kabisa bungeni, amemtuhumu Netanyahu kwa kile alichokiita "uzembe wa kisiasa." Amesema, hakuna anemuamini tena waziri mkuu.

Serikali ya waziri mkuu wa zamani wa Israel,Ehud Olmert wa chama cha Kadima, ndio iliyoanza kuiwekea vikwazo Gaza. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya mwanajeshi wa Kiisraeli Gilad Shilat, kutekwa nyara na kupelekwa Ukanda wa Gaza na wanamgambo wa Kipalestina, miaka minne iliyopita. Mwaka mmoja baadae,vikwazo hivyo viliimarishwa dhidi ya Hamas, baada ya chama hicho kutumia nguvu kulidhibiti eneo la Gaza Juni mwaka 2007.

zu unserem KORR Nahost/Gaza/Israel: **ARCHIV** Israeli Prime Minister Benjamin Netanyahu speaks after a meeting with Canadian Prime Minister Stephen Harper in Ottawa, Canada, Monday May 31, 2010. (AP Photo/The Canadian Press, Adrian Wyld)
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.Picha: AP

Waziri Mkuu Netyanyahu akiitetea sera yake mpya kuhusu Ukanda wa Gaza amesema, serikali itaruhusu bidhaa zote kuingia Gaza isipokuwa silaha na zana zinazoweza kutumiwa kutengenezea silaha. Idadi ya bidhaa zitakazoruhusiwa Gaza itaongezeka kwa asilimia 30. Alipohotubia kamati ya sera za nje na ulinzi katika bunge la Israel,Netanyahu alisema:

" Kwanza kabisa,sera yetu ni kuwalinda raia wa Israel dhidi ya ugaidi na mashambulio ya makombora kutoka Gaza."

Lakini kwa maoni ya chama cha Hamas kinachodhibiti eneo la Gaza, hatua ya kuregeza vikwazo haitoshi. Chama hicho kinataka uhuru kamili wa kusafirisha bidhaa na vile vile vikwazo vya baharini viondoshwe.

Wakati huo huo, Waziri wa Misaada ya Maendeleo wa Ujerumani,Dirk Niebel aliekuwa ziarani Israel amesema, uamuzi wa serikali ya nchi hiyo kuregeza vikwazo utekelezwe kikamilifu. Hapo awali,Israel ilimnyima waziri Niebel ruhusa ya kuingia Ukanda wa Gaza.

Mwandishi:Engelbrecht,Sebastian/ZPR/P.Martin

Mhariri:Liongo,Abubakar