1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa upinzani Odinga anataka uchaguzi mpya Kenya

Sekione Kitojo
29 Oktoba 2017

Akionya kuwa Kenya imo katika "hatari  kubwa", kiongozi wa upinzani Raila Odinga amesema katika  mahojiano Jumapili (29.10.2017) kwamba uchaguzi mpya wa rais ulikuwa hauna maana na uchaguzi mpya ufanyike katika siku 90.

https://p.dw.com/p/2mheC
Kenia Nairobi Opposition ehemailger Präsident Raila Odinga
Picha: Reuters/B. Ratner

Idadi  ndogo  ya watu waliojitokeza  kupiga  kura  katika  uchaguzi wa Alhamis, ukiwa  ni  uchaguzi  mpya  wa  rais , baada  ya  ule  uliofanyika mwezi  Agosti , inaonesha  kwamba  mchakato  mzima  wa  uchaguzi ni  batili, na  serikali  ya  rais  Uhuru  Kenyatta  inajaribu "kuharibu taasisi  nyingine za utawala  nchini," ikiwa  ni  pamoja  na  mahakama  kuu, Odinga amesema. Alisusia uchaguzi , akisema  mageuzi  ya  uchaguzi  yanahitajika.

Kenia Raila Odinga bei Kundgebung in Mombasa
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila OdingaPicha: Reuters/J. Okanga

Odinga  alizungumza  na  shirika  la  habari  la  AP baada  ya  makabiliano yaliyosababisha  umwagikaji  wa  damu  kati  ya  polisi na  waungaji  mkono wa  upande  wa  upinzani  katika  baadhi  ya  sehemu  za  Kenya  tangu uchaguzi  huo  kufanyika, pamoja  na  kuahirishwa  kwa  uchaguzi katika maeneo  ambayo  ni  ngome  kuu  za  upinzani  ambako  vituo  vya  kupigia kura  havikuweza  kufunguliwa  kwasababu ya  matatizo  ya  kiusalama.

Mahakama  kuu  ilibatilisha  uchaguzi  wa  hapo Agosti 8, baada  ya kugundua  kile  ilichosema  kuwa  ni  mapungufu  na  kutokuwa  na  uhalali, na kusababisha ukosoaji  mkali kutoka  kwa  rais  Kenyatta, ambaye  alitangazwa mshindi  katika  uchaguzi  huo.

"Nchi yetu imo katika hatari kubwa," amesema  Odinga, licha kukiri kuwa tayari  kwa  majadiliano  na  kambi  ya  Kenyatta  juu  ya  kufanyika  kile alichokiita  uchaguzi  huru  na  wa  haki.

Kenia Kisumu Proteste
Maandamano yaliyoambatana na ghasia katika maeneo ya upinzani katika mji wa KisumuPicha: picture-alliance/dpa

"Sisi  sio  kwamba  hatuko  tayari  kwa  mazungumzo  lakini  ajenda  bado itakuwa ile  ile , jinsi  gani  ya  kuweka  uwanja  sawa  ili  uchaguzi  uweze kufanyika  katika  muda  wa  siku 90," Odinga  alisema   katika  mahojiano yaliyofanyika  nyumbani  kwake  mjini  Nairobi.  " Hiki  ndio tutakuwa  tayari kukijadili  na  wao."

Matokeo ya awali

Matokeo  ya  awali  kutoka  vituo  vya  kupigia  kura  ambayo  yamewekwa katika  tovuti  ya  tume  ya  uchaguzi  na  mipaka  ya  Kenya   yanaonesha kwamba  Kenyatta  amepata  kura  nyingi  katika  maeneo  mengi  baada  ya uchaguzi  wa  hapo Alhamis. "Kimsingi  ilikuwa  Uhuru  dhidi  ya  Uhuru," Odinga  amesema.

Wakati  huo  huo  mkuu  wa  tume  ya  uchaguzi  nchini  Kenya  Wafula Chebukati alitarajiwa  kutangaza  leo iwapo uchaguzi utaendelea  katika maeneo yaliyozuka  ghasia  ya  upinzani, ambako  ususiaji umezusha maandamano  ya  ghasia  katika  uchaguzi  ambao unatarajiwa  kumpa  Uhuru Kenyatta  ushindi  wa  kishindo , lakini wenye  dorasi.

Wakati  zoezi  la  kuhesabu  kura  likiwa  karibu  limekamilika baada ya uchaguzi  wa  hapo Alhamis , matokeo  bado  hayajatangazwa  rasmi wakati maafisa  wakitafakari kile  cha  kufanya  juu  ya  majimbo 25  ya  kupiga  kura ambako  uchaguzi  ulizuiwa.

Kenia - Wahlen - Vorsitzender des Independence Electoral and Boundaries Commission Wafula Chebukati bei Pressekonferenz
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya Wafula ChebukatiPicha: picture-alliance/AP Photo/S. A. Azim

Katika  maeneo  hayo, waungaji  mkono  wa  kiongozi  wa  upinzani Raila Odinga  walifanikiwa  kuzuwia  mamia  ya  vituo  vya  kupigia  kura kufunguliwa, na  kusababisha  makabiliano ya  vurugu  na  polisi ambayo yaliendelea  kwa  siku  kadhaa, na  kusababisha  watu tisa  kuuwawa  na wengine  kadhaa  wamejeruhiwa.

Kiasi  ya  watu  49 wameuwawa  tangu uchaguzi  wa  kwanza  wa  rais Agosti 8, ambao baadaye  ulibatilishwa, na  kusababisha  mzozo  mkubwa  wa kisiasa nchini  Kenya  katika  muongo  mmoja.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / ape

Mhariri: Yusra Buwayhid