1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa upinzani Urusi afikishwa mahakamani

Isaac Gamba
27 Machi 2017

Kiongozi wa upinzani nchini Urusi Alexei Navalny amefikishwa mahakamani leo Jumatatu tarehe (27.03.2017) siku moja baada ya kiongozi huyo pamoja na wafuasi wake wengine kutiwa mbaroni.

https://p.dw.com/p/2a0zr
Russland Nawalny Festnahme bei den Protesten in Moskau
Picha: picture-alliance/AP Photo/Evgeny Feldman for Alexey Navalny's campaign

 Kukamatwa kwa kiongozi huyo wa upinzani kunafuatia maandamano yaliyofanyika jana Jumapili kupinga rushwa na  ambayo ni makubwa  tangu yale ya mwaka 2011/2012 na yamefanyika ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya kuitishwa uchaguzi wa Rais ambao Rais wa sasa Vladimir Putin anatarajiwa kuwania tena nafasi hiyo ukiwa ni muhula wake wanne.

Utafiti wa maoni unaonyesha kuwa upinzani wa kileberali unaowakilishwa na Navalny una nafasi ndogo ya kuweka mgombea mwenye uwezo wa kumuondoa madarakani Rais Putin anayepewa nafasi kubwa kusalia madarakani.  Hata hivyo Navalny na wafuasi wake wanatarajia kuvuta hisia za umma kuhusiana na hoja yao ya kupinga vitendo vya rushwa.

Mwandishi wa habari wa gazeti la Reuters alishuhudia polisi wakimakamata Navalny anayetarajia kushindana na Rais Putin kwenye kinyan'ganyiro hicho wakati alipokuwa akitembea katika mitaa ya mjini Moscow na wafuasi wake mnamo wakati helikopta ilipokuwa ikizunguka eneo hilo.

Polisi walimuingiza Navalny ndani ya lori  lililokuwa limezungukwa na mamia ya waandamanaji wakijaribu kufungua milango ya lori hilo.

"Nina furaha kuwa watu wengi wamejitokeza katika mitaa kutoka mashariki mwa nchi hadi mjini Moscow" alisikika Navalny kabla hajakamatwa. Ikulu ya Urusi - Kremlin, ilisema maandamano ya mjini Moscow yaliyopigwa marufuku na mamlaka ya mji huo yalifanyika kinyume cha sheria.

Marekani yataka waandamanaji waliokamatwa waachiwe huru

USA Mark Toner
Mark Toner msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya MarekaniPicha: U.S. Department of State.

Marekani imelaani kukamatwa kwa waandamanaji hao na kusema hatua hiyo inakiuka misingi ya demokrasia.  Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Mark Toner katika taarifa yake alisema Marekani inatoa mwito kwa serikali ya Urusi kuwaachia mara moja waandamanaji waliotiwa mbaroni na kuongeza kuwa imesikitishwa na kukamatwa  kiongozi wa upinzani Navalny.

Polisi wanasema  watu kati ya 7,000 na 8,000 walikuwa wamekusanyika katika mtaa wa Tverskaya na maeneo yanayozunguka eneo hilo na kuitaja idadi ya watu waliokuwa wamekamatwa kufikia jana jioni kuwa 500.

Kiongozi wa upinzani Navalny aliitisha maandamano hayo baada ya kuchapisha taarifa kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Medvedev  ana miliki mali nyingi ambazo haziendani na mshahara wake anaopokea kwa mwezi.

Msemaji wa Medvedev ameyaita madai hayo kuwa ni mashambulizi ya propaganda dhidi ya kiongozi huyo na kuongeza kuwa yanalenga kuchafua jina lake katika kipindi hiki cha kuelelekea uchaguzi.

Kwingineko katika mji wa mashariki wa Vlaivostok, mwandishi wa shirika la habari la Reuters alishuhudia watu 30 wakikamatwa baada ya kuonyesha bango lililosomeka  " Waziri Mkuu lazima ajibu"

Vyombo vya habari nchini humo viliripoti kuwa maandamano makubwa pia yalifanyika katika miji mingine ikiwa ni pamoja na St Petersburg na Novosibirsk. Hata hivyo vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali vilipuuza kwa kiwango kikubwa maandamano hayo ya jana.

Mwandishi: Isaac Gamba/rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga