1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa upinzani Zambia Hichilema aachiliwa huru

John Juma
16 Agosti 2017

Kiongozi wa upinzani nchini Zambia, wa chama cha UPND, Hakainde Hichilema aliachiliwa huru Jumatano baada ya kiongozi wa mashtaka nchini humo Bibi Lillian Siyunyi kuyaondoa mashitaka ya uhaini dhidi yake.

https://p.dw.com/p/2iMBx
Sambia Hakainde Hichilema
Picha: Getty Images/AFP/D. Salim

Mahakama kuu nchini Zambia imefutilia mbali kesi ya uhaini dhidi ya kiongozi wa upinzani nchini humo Hakainde Hichilema na kumuachilia huru na wenzake watano. Hii ni baada ya kiongozi wa mashtaka kuyaondoa mashtaka dhidi ya Hichilema bila ya kutoa sababu maalum.

Kiongozi wa upinzani wa chama cha Umoja kwa Maendeleo ya Kitaifa nchini Zambia, UPND, Hakainde Hichilema aliachiliwa huru leo baada ya kiongozi wa mashtaka nchini humo Bibi Lillian Siyunyi kuiambia mahakama ya Lusaka kuwa anaondoa mashitaka dhidi ya Hichilema pamoja na maafisa wengine watano wa chama chake ambao wote walikanusha tuhuma za uhaini dhidi yao. Upande wa mashtaka haukutoa sababu za kuyaondoa mashtaka hayo.

Hofu ya kukamatwa kwake tena

Msemaji rasmi wa chama cha upinzani cha National Restoration Party, Narep Bwalya Nondo, amesifia kuachiliwa huru kwa Hichilema, lakini angali anahofu kuwa Hichilema angali anaweza kupokonywa uhuru wake.

"Tunayofuraha kuwa mwenzetu ameachiliwa kutoka jela, lakini tunahuzunika kuwa hana uhuru kwa sababu wasilisho la serikali mahakamani halimruhusu mshukiwa yeyote wa uhalifu kuwa na uhuru kamili, anaweza kukamatwa tena kwa mashtaka hayohayo na arudishwe mahakamani. Ndiyo sababu tunataka serikali kufutilia mbali kesi hiyo kwa manufaa ya Amani na upatanisho wa dhati ili taifa lifungue ukurasa mpya."

Alizuia msafara wa rais Lungu

Afisa wa polisi mbele ya wafuasi wa Rais Lungu katika kampeni za mwaka 2016
Afisa wa polisi mbele ya wafuasi wa Rais Lungu katika kampeni za mwaka 2016Picha: Getty Images/AFP/G. Guercia

Hichilema alikamatwa mwezi Aprili mwaka huu na kushtakiwa kwa uhaini kufuatia kisa cha msafara wake kutouachilia njia msafara wa Rais Edgar Lungu na akalaumiwa kwa kuhatarisha maisha ya rais kwa lengo la kuchukua mamlaka.

Kesi hiyo ya uhaini ilikuja baada ya Hichilema kushindana na Rais Lungu katika uchaguzi wa urais mwaka uliopita ambapo Lungu alitangazwa mshindi kwa asilimia 50 ya kura dhidi ya 47 ya Hichilema.

Baadaye Hichilema aliwasilisha kesi ya kupinga ushindi wa Lungu mahakamani. Baadhi ya wafuasi wake walijitokeza nje ya mahakama kuelezea furaha yao. Patricia Banji ambaye ni mwenyekiti wa jinsia katika chama cha UPND ni mmoja wao.

"Ninayo furaha hata naweza kuongea sana kw akuona rais wetu na hili ndilo tumekuwa tukisubiri kwa muda mrefu. Tulijua siku moja rais wetu ataachiliwa huru. Leo Zambia na dunia kwa jumla inafuraha kwa kumuona rais wetu yuko huru."

Wito wa wafungwa wa kisiasa kuachiliwa huru

Afisa wa uchaguzi wa Zambia akibeba karatasi ya kura
Afisa wa uchaguzi wa Zambia akibeba karatasi ya kuraPicha: Getty Images/AFP/D. Salim

Muda mchache baada ya kuachiliwa kwake, mwenyewe Hichilema aliitolea wito kuwaachia huru wafungwa wengine wote wa kisiasa walioko magerezani.

Kwa miaka mingi, taifa hilo la Afrika Kusini limeshuhudia upokezanaji wa mamlaka kwa njia ya amani na hata kusifiwa na Umoja wa Mataifa kama mfano bora kwa Afrika. Lakini katika uchaguzi uliopita, kulitokea ghasia za kisiasa.

Makundi ya kutetea haki za kibinadamu yalitaja kesi dhidi ya Hichilema kama hatua ya kunyamazisha sauti za wapinzani

Zambia imekuwa katika hali ya tahadhari tangu mwezi Julai mwaka huu kufuatia ghasia na taharuki zilizoshuhudiwa. Hali hiyo ya tahadhari inatarajiwa kudumu hadi mwezi Oktoba. Rais Lungu ametaja vurugu hizo kuwa njama za kuvuruga uchumi wa nchi.

Mwandishi: John Juma/ APAE/DPAE
Mhariri: Mohammed Khelef