1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kisa cha Kundus magazetini

Oumilkher Hamidou14 Desemba 2009

Eti kweli waziri wa ulinzi ataangukia mhanga wa kisa alichoachiwa na mtangulizi wake?

https://p.dw.com/p/L1pk
Majeruhi wa shambulio la mabomu dhidi ya malori ya mafuta huko KundusPicha: dpa

Kisa cha kushambuliwa kwa mabomu malori ya mafuta katika mji wa kaskazini wa Afghanistan -Kundus,kimehanikiza magazetini hii leo.Mbali na mada hiyo wahariri wamemulika pia mkutano wa hifadhi ya hali ya hewa mjini Copenhagen .Tuanzie lakini Berlin ambako siri kuhusu chanzo cha kushambuliwa malori ya mafuta huko Kundus zinazidi kufichuliwa.Gazeti la "RHEIN-ZEITUNG" linaandika:

Ikiwa baada ya kumuachisha kazi Franz Josef Jung,kansela Angela Merkel atalazimika pia kumtoa mhanga,waziri anaependwa na wengi ,hapo serikali ya muungano wa nyeusi na manjano itazongwa na mzozo mkubwa.Lakini hali hii haijaripuka vivi hivi.Tatizo hili linatokana na mtindo wa kisiasa wa kansela Merkel:Mtindo wa kuanyamaza matatizo yanapochomoza.Hata katika kadhia ya Kundus,kansela Merkel alijaribu kuzinyamazia lawama zilizokua zikitolewa.Hilo lilikua kosa kubwa.Kwasababu hivi sasa anajikuta akitupiwa dhana ya kulidanganya bunge.Angebidi atambue tangu zamani kwamba usukani wa kisa hicho umo mikononi mwa vyombo vya habari na sio tena serikalini.Analazimika hivi sasa kubadilisha hali ya mambo, la sivyo,hata kiti chake kitatikisika.

Gazeti la "KIELER NACHRICHTEN"

linaandika:

Madai ya upande wa upinzani kumtaka waziri wa ulinzi ajiuzulu,yametolewa kwa pupa.Kwasababu hadi wakati huu bado hoja zinazotolewa zinapingana.Lakini kwa kadiri fulani,mwenyekiti wa chama cha upinzani cha SPD, Sigmar Gabriel hajakosea aliposema zu Guttenberg atumiliwe wezani ule ule aliotumiliwa mtangulizi wake Franz Josef Jung.

Gazeti la HANNOVERSCHE ALLGEMEINE ZEITUNG linahisi kuna kitu kinachofichwa nyuma ya lawama za upande wa upinzani.Gazeti linaendelea kuandika:

Lawama dhidi ya waziri wa ulinzi zinafichua baadhi ya mambo kutoka upande wa upinzani.Anaesikiliza kwa makini hakosi kugundua nahau ya aina mpya ya Sigmar Gabriel.Kiongozi wa chama cha SPD analenga mageuzi ya siasa za Ujerumani kuelekea Afghanistan.Kikijikwamua toka adha ya kuwa mshirika katika serikali ya muungano,chama cha SPD kinachoongozwa na Sigmar Gabriel kinataka kubadilisha msimamo wake kuelekea kuwepo vikosi vya Ujerumani Bundeswehr nchini Afghanistan-mpango ambao tokea hapo hauungwi mkono na wananchi walio wengi.Chanzo na madhara ya mashambulio ya Kundus yanampatia hoja za kutosha mwenyekiti mpya wa chama cha SPD.Kama zu Guttenberg anavyojaribu kujitenganisha na mtangulizi wake ,ndivyo nae Gabriel anavyojaribu kufuata mkondo mpya.

Demonstrationen in Kopenhagen
Waandamanaji wahimiza makubaliano yafikiwe mjini CopenhagenPicha: AP

Mada yetu ya pili na ya mwisho inahusu mkutano wa hifadhi ya hali ya hewa mjini Copenhagen.Gazeti la "FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG" linaandika

Kauli mbiu ya kudai ulimwengu wa haki,imesalia vile vile kwa miongo sasa.Sema safari hii kuna kifungu ziada:Hali ya hewa.Ndio maana mjini Copenhagen kunazungumziwa kuhusu haki sawa,mshikamano,wema na waovu,maskini na tajiri na pia hali ya hewa.Hali hiyo inatajwa linapohusika suala la kusawazisha mzigo unaozielemea nchi zinazoinukia kufuatia juhudi za kuhifadhi hali ya hewa.Na sasa pia sio mabadiliko ya hali ya hewa yatakayo sahihisha fedha ziada za misaada ya maendeleo,bali namna ya kuziba pengo kati ya neema na ufukara."

Mwandishi Hamidou Oummilkheir (Inlandspresse)

Mhariri: Abdul-Rahman