1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kisa cha madai ya rushwa nchini Israel:Barak amtaka Waziri mkuu Olmert ajiuzulu

Abdulrahman, Mohamed28 Mei 2008

Asema la sivyo chama chake kitashinikiza uchaguzi wa mapema

https://p.dw.com/p/E7hm
Waziri wa ulinzi na mkuu wa chama cha Leba nchini Israel Ehud Barak.Picha: AP

Waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak leo amemtaka Waziri mkuu Ehud Olmert ajiuzulu na kumkabidhi madaraka mtu mwengine kutoka chama chake cha Kadima au awe tayari kwa uchaguzi mkuu wa mapema. Hatua ya Bw Barak ambaye chama chake cha Leba ni mshirika mkubwa katika serikali ya mseto ya Bw Olmert,imekuja siku moja baada ya Bw Olmert kuungama kwamba alipokea dola 150.000 kutoka kwa mfanyabiashara mmoja , lakini akakana kwamba haikua hongo bali mchango halali kwa ajili ya kampeni ya uchaguzi.

Akizungumza na waandishi habari kwenye jengo la bunge Knesset leo, Bw Barak ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Leba alisema kwamba.Waziri mkuu Olmert ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Kadima kinachounda serikali ya mseto pamoja na Leba, anaweza kujiondoa mwenyewe ama kwa kujiuzulu au kujiweka kando kwa muda na kukitaka chama cha Kadima kumteuwa kiongozi mwengine ashike wadhifa wake.

Akasisitiza kwamba hili halina budi lifanyike haraka, la sivyo akaongeza Bw Barak, basi chama cha Leba kitapigania paitishwe uchaguzi wa mapema. Akizungumza kile alichokiita changamoto inayokabiliana nayo Israel wakati huuo, akaongeza,"Kutokana na hali ya sasa kuhusiana na changamoto ambayo Israel inakabiliana nayo ikiwa ni pamoja na chama cha Hamas, Hizbollah, Syria na Iran, pamoja na suala la wanajeshi wake wanaoshikiliwa mateka na mahasimu wao na mwenendo mzima wa amani, Waziri mkuu Olmert hawezi kuiongoza serikali na kushughulikia masuala yake ya binafsi ,wakati mmoja."

Bw Barak ambaye 1999 binafsi alikabiliwa na uchunguzi kuhusu kugharimiwa kifedha kwa kampeni yake ya uwaziri mkuu, alisema kuondoka kwa Olmert madarakani litakua ni suala litakalokubalika kwa heshima. Lakini hata kabla ya Barak kutangaza hayo, mshauri wa Bw Olmert, Tal Zilberstein alisema Waziri mkuu huyo hatojiuzulu kwa sababu kufanya hivyo kutakua ni sawa na kukiri kuwa ana hatia.

Sakata hili jipya limekuja baada ya mfanyabiashara anayeishi Newyork Morris Talansky kuungama jana kwamba alimpa Bw Olmert fedha hizo ambazo alisema hazikulipwa miaka 15 iliopita.

Vuguvugu la kumtaka Bw Olmert ajiuzulu limo paia ndani ya cahama chake bifasi cha Kadima. Itakumbukwa Mei mwaka jana Waziri wake awa mambo ya nchi aza nje Bibi Tzipi Livni pia alimtaka Waziri mkuu huyo ajiuzulu baada ya kukosolewa vikali katika ripoti ya muda jinsi serikali ilivyovishughulikia vita vya 2006 nchini Lebanon.

Wakati huo huo Mamlaka ya utawala wa wapalestina imeeelezea wasi wasi wake kwamba mgogoro wa kisiasa nchini Israel unaweza kuhujuma mwenendo wa mazungumzo baina ya Israel na wapalestina. Msemaji wa rais Mahmoud Abbas, Nabil Abu Rudeina alisema pamoja na hayo hilo ni suala la ndani la Israel, lakini kilicho muhimu kwao ni kuona waziri mkuu yeyote wa Israel anajitolea kwa moyo thabiti katika utaratibu wa kusaka amani ya Mashariki ya kati.

Mazungumzo hayo yalianza Novemba baada ya kukwama kwa karibu miaka 7, huku pakiwekwa matumaini ya kuweza kufikia makubaliano ifikapo mwishoni mwa mwaka huu juu ya suala la kuundwa dola ya wapalestina.