1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Ukraine

21 Januari 2015

Jinsi ya kukabiliana na kitisho cha mashambulio ya kigaidi,hali nchini Ukraine na kongamano la kiuchumi mjini Davos Uswisi ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/1ENfT
Kesi dhidi ya mtuhumiwa msaidizi wa wanamgambo wa kigaidi Harun P.mjini MunichPicha: picture-alliance/dpa/S. Widmann

Tuanzie lakini na juhudi za kukabiliana na kitisho cha mashambulio ya kigaidi. Gazeti la "Rhein-Zeitung" linaandika:"Siku chache baada ya shambulio la Ufaransa, bila ya shaka hata idara za usalama nchini Ujerumani ziko katika hali ya taharuki. Hata hivyo uamuzi wa polisi ya Dresden ambao hautaji siku gani hasa kitisho hicho kitatokea,usiachiwe kugeuka funzo.Kwamba katika hali ya kitisho kikubwa ambacho "hakijabainika",mikusanyiko ya watu ipigwe marufuku-hilo lisiachiwe.Jamii iliyo huru inabidi ijifunze namna ya kuishi na kitisho ambacho si bayana. Wafuasi wa vuguvugu la Pegida ndio waliofaidika zaidi na marufuku hayo. Wanasiasa kutoka vyama vyote vya kisiasa wameelezea umuhimu kwa vuguvugu hilo linalobishwa kuendelea na maandamano yao.Marufuku hayo yamewapatia Pegida uangalifu ambao hawajaustahiki. Viongozi wao wanajigeuza wahanga hivi sasa wakitegemea kujipatia umasuhuri mkubwa zaidi kutokana na maandamano yao ya karaha.

Shida katika maeneo ya Mashariki ya Ukraine

Hali nchini Ukraine nayo pia imechambuliwa magazetini. Gazeti la "Thüringische Landeszeitung" linaandika:"Zaidi ya hayo kuna shida kubwa katika maeneo ya mashariki ya Ukraine yanayodhibitiwa na waasi.Msimu wa baridi umewazidishia matatizo watoto,wazee,na familia kwasababu waasi waliojitenga na serikali ya mjini Kiev wanashindwa kudhamini mfumo madhubuti wa huduma za jamii.Kuna ukosefu wa chakula,mitambo ya kuzipasha moto nyumba,madawa,maji na kadhalika.Silaha tu ndio zilizojazana.Kiroja lakini ni pale kiongozi wa waasi anapozungumzia maandalizi ya vita.Nani aliyetwaa silaha katika nchi hiyo ambayo awali ilikuwa ya amani na kulitenga eneo kubwa la nchi hiyo badala ya kuketi na kujadiliana?Kwa kutamka hivyo wanataka kuwatupia wengine tu dhamana ya yanayotokea.!

Viongozi wa dunia wakutana Davos

Na ripoti yetu ya mwisho magazetini inahusu kongamano la kiuchumi la kimataifa mjini Davos. Gazeti la "Landeszeitung" linaandika: "Mara moja kwa mwaka mji tulivu wa Davos unageuka kitovu cha madaraka.Hakuna mahala kokote kwengine duniani ambako viongozi wengi kabisa wa serikali, wataalam mashuhuri wa kiuchumi na wasomi wanakutikana wameketi pamoja kama inavyoshuhudiwa wakati huu tulio nao katika kongamano hili la kiuchumi la kimataifa. Kongamano hili kubwa lilijiwekea lengo la kuibadilisha hali ya mambo duniani na kuifanya iwe bora.Mtu akitafakari hii leo basi hatokosa kutambua tangu mwaka 1971,hakuna mengi yaliyotokea.Kwa upande mmoja imezuka mizozo mfano wa ule wa Ukraine,Iraq, na Syria na kwa upande wa pili matatizo kadhaa bado hayajapatiwa ufumbuzi:njaa,umaskini na maradhi kwa mfano. Zaidi ya hayo imezuka migogoro ya kiuchumi inayozidi kulipanua pengo kati ya jamii zenye tamaduni tofauti na mabadiliko ya tabia nchi yanayoatia hatarini maisha ya mamilioni ya watu.Davos ingebidi igeuka kongamano la kusaka ufumbuzi wa matatizo hayo,badala ya kuwa kongamano la mivutano."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Iddi Ssessanga