1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kitisho cha nyuklia Japan

22 Machi 2011

Wahandisi nchini Japan leo wamekuwa na kazi ngumu ya kushughulikia tena mifumo ya upozaji katika kiwanda cha nyuklia cha Fukushima baada ya kitisho cha kufuka moshi mpya, huku kukiwa kumegunduliwa mionzi katika bahari.

https://p.dw.com/p/10fAx
Msemaji wa serikali ya Japan, Yukio EdanoPicha: picture alliance / dpa

Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Usalama wa Nyuklia na viwanda nchini Japan Hidehiko Nishiyama amesema bado kuna kiwango kidogo cha moshi mweupe unaotoka katika mtambo namba mbili.

Hata hivyo amesema hakuna tena moshi unaotoka katika mtambo namba tatu.

Tayari umeme wa nje umerudishwa katika mtambo wa tano na wa sita, baada ya siku 11 tangu tsunami kuuharibu kiwanda hicho, lakini hata hivyo  kazi zaidi inahitajika kabla ya umeme kurudi katika eneo hilo.

Hofu kubwa inayolikabili taifa hilo kwa sasa  ni kitisho kisichoonekana kutokana na mionzi inayovuja kutoka katika mtambo namba moja, ambao uko kilomita 250 katika mji mkuu wa Tokyo ambao unakaliwa na wakaazi wapatao milioni 30.

Kufuatia kitisho hicho kipya kilichojitokeza, serikali nchini Japan imesimamisha usafirishaji wa baadhi ya vyakula katika maeneo yaliyokaribu na kinu hicho baada ya kugundulika kiwango cha juu cha mionzi kuliko ilivyo kawaida katika na maziwa.

Mapema leo wizara ya Afya nchini humo imeagiza kuongezwa kwa ukaguzi katika vyakula vya baharini baada ya dalili za mionzi kugunduliwa katika bahari ya Pacific jirani na kiwanda hicho cha Fukushima.

Na katika hatua nyingine uhaba wa mafuta, mvua ya barafu  na tatizo la umeme limekuwa ikikwamisha juhudi zinazochukuliwa kupambana na msukosuko mbaya wa kibinadamu kuwahi kuikumba nchi hiyo tangu kutokea kwa vita kuu ya pili ya dunia, licha ya wafanyakazi wa misaada kuripoti kufanikiwa kiasi, huku barabara zilizoharibika zikianza kutumika tena na ujenzi wa nyumba mpya.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu masuala ya kiutu, mvua imekuwa ikikwamisha juhudi za ugawaji wa misaada kwa kutumia helikopta na kusababisha mamlaka husika kuanza kutumia tena barabara na kusababisha misaada hiyo kuchelewa.

Akizungumzia hali ilivyo sasa nchini Japan Francis Markus kutoka Shirika la Kimataifa la msalaba mwekundu na hilali nyekundu amesema kumekuwa na maendeleo kiasi katika suala la mpangilio wa ugavi wa chakula na usafirishaji  wa watu na vitu pamoja na kupata chakula na mahitaji mengine.

Hata hivyo amekiri kuwa hali bado ni mbaya.

Aidha mpaka sasa bado haijafahamika ni watu wangapi wameweza kufikishiwa misaada inayogaiwa katika maeneo hayo yaliyokumbwa na tsunami, wakati uhaba wa mafuta pia ukichangia kuzuia misaada kufika katika maeneo ya vijiji vya mbali.

Tetemeko baya la ardhi na janga la Tsunami lililoikumba nchi hiyo limesababisha watu 319,000 kuhamishwa kutoka kwenye makaazi yao.

Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters, afp)

Mhariri Yusuf Saumu Ramadhani