1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kitisho cha ugaidi Ujerumani na Austria

Mohammed Abdul-Rahman12 Machi 2007

Wanaharakati wa Kiislamu wadai kutekeleza ugaidi pindi nchi hizo mbili hazitawaondoa wanajeshi wao Afghanistan.

https://p.dw.com/p/CB5K

Serikali ya Ujerumani inazitathimini kwa undani taarifa kwamba wanaharakati wa Kiislamu wametishia kuzishambulia Ujerumani na Austria ikiwa hazitowaondoa wanajeshi wao nchini Afghanistan. Taarifa hiyo ilisomwa jana kwenye mtandao mmoja wenye mafungamano na kundi la Al-Qaeda na watu waliojifunika nyuso zao , wakati kwa upande mwengine mwanamke mmoja wa Kijerumani na mwanawe wa kiume waliotekwa nyara nchini Irak wakiendelea kushikiliwa.

Taarifa hiyo katika kanda ya video,ilisema kwamba kushiriki kwa Ujerumani katika vita vya Marekani dhidi ya Uislamu na Waislamu, kutaihatarisha Ujerumani binafsi. Waliohusika na taarifa hiyo hawakuweza kufahamika, lakini kundi hilo linajiita Kataeb Siham al-haq (Mishale ya haki ) Sambamba na hayo msemaji, anasikika akiongeza “Kwa kusimama upande wa Marekani, umewachochea wale unaowaita magaidi, wakugeuze uwe shabaha yao.” Matamshi hayo kwa lugha ya kiarabu yalikua na tafsiri ya maandishi kwa lugha ya Kijerumani.

Ujerumani ina karibu wanajeshi 3,000 katika eneo la kaskazini mwa Afghanistan ambalo kwa sehemu kubwa ni lenye utulivu-mahala ambako inakiongoza kikosi cha kimataifa kilichoko huko. Taarifa ya hapo jana ilitishia kuishambulia pia Austria iwapo nayo haitowaondoa wanajeshi wake kutoka Afghanistan.

Tukio hilo limekuja katika wakati ambao mama mmoja wa Kijerumani na mtoto wake wa kiume wakiendelea kushikiliwa baada ya kutekwa nyara nchini Irak. Serikali ya Ujerumani ilithibitisha tarehe 12 ya mwezi uliopita, kwamba raia wawili wa Ujerumani wamepotea nchini Irak na wakati huo ilikua tayari ni wiki moja tangu walipotoweka.

Wanaharakati wanaowashikilia mateka watu hao wawili, wametishia kuwauwa ikiwa Ujerumani haitowaondoa wanajeshi wake Afghanistan katika muda wa siku 10. Katika mkanda wa video uliotumwa na wateka nyara kwenye mtandao mmoja wa wanaharakati wa Kiislamu, mama huyo wa miaka 61, anaonekana huku akitokwa machozi, akimuomba Kansela Angela Merkel kuwasaidia yeye na mwanawe akisema “ sisi pia ni wajerumani. Watu hawa wanataka kumuuwa mwanangu mbele ya macho yangu na baadae kuniuwa na mimi. Sitaki kufa namna hii .”.

Mjini Berlin waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeir akasema, “Tutafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanarudi Ujerumani wazima na kujiunga tena na familia yao.”

Awali msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje mjini Berlin alisema, jopo lililoundwa na serikali baada ya utekaji nyara huo, unaizingatia hali ya mambo ikiwa ni pamoja na kuichunguza taarifa ya kitisho cha mashambulio dhidi ya Ujerumani.

Wakati wanaharakati hao wa Kiislamu nchini Irak wakiunganisha utekaji nyara huo wa karibuni na dai la kutaka wanajeshi wa Ujerumani na Austria waondoke Afghanistan, huko Irak kwenyewe umwagaji damu unaendelea., baada ya watu 41 kuuwawa mwishoni mwa juma, hali inayoashiria mafanikio ya kampeni ya usalama ya majeshi ya Marekani katika mji mkuu Irak mjini Baghdad yamekua ya ni kiwango fulani tu.

Kwa mujibu wa ripoti ya kijeshi, wanajeshi wengine 4 wa Marekani wameuwawa, wawili katika mabambano na wawili wengine katika matukio ambayo hayakufafanuliwa. Vifo vyao vimeongeza idadi ya wanajeshi wa Marekani waliouwawa tangu uvamizi wake nchini Irak 2003 na sasa kufikia 3,196.