1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kivu, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Watu 17 wauwawa.

28 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBxV

Kiasi watu 17 wamepigwa marungu na kukatwa mapanga na kufa na watu wanaosadikiwa kuwa ni waasi kutoka Rwanda katika jimbo la mashariki la Kivu kusini katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.

Watu wengine 28 wanaripotiwa kuwa wamejeruhiwa na watu wengine 12 wametekwa nyara katika shambulio hilo ambalo lilifanyika jioni ya Jumamosi dhidi ya vijiji viwili.

Jeshi la umoja wa mataifa la kulinda amani na lile la Kongo wamefanya operesheni ya pamoja wiki kadha zilizopita katika eneo hilo dhidi ya wapiganaji kutoka katika kundi linalojiita Democratic Forces for the Liberation of Rwanda, kundi ambalo ni la Wahutu lililoko mashariki ya Kongo.

Licha ya kumalizika rasmi kwa vita vya mwaka 1998-2003 vya wenyewe kwa wenyewe, majimbo ya mashariki ya Kongo mara kwa mara yanashuhudia ghasia zinazofanywa na wanamgambo wa eneo hilo, makundi ya waasi kutoka nje ya nchi hiyo , pamoja na majeshi ya ulinzi ya nchi hiyo.