1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiwango cha hatari chapandishwa baada ya shambulio London

Sekione Kitojo
16 Septemba 2017

Uingereza  imepandisha kiwango cha  kitisho cha mashambulizi ya  kigaidi, ikiwa  na  maana  kwamba shambulio jingine  linaweza kutokea wakati wowote.

https://p.dw.com/p/2k5Kj
London Anschlag auf Underground Ubahn
Picha: picture alliance/AP Photo

Kundi linalojiita  "Dola la  Kiislamu" limesema  linahusika  na shambulio  hilo ambalo watu 29 wamejeruhiwa  katika  kituo cha treni kilichokuwa na watu wengi cha chini  ya  ardhi mjini London.

Polisi ya Uingereza imeanza kazi ya kumtafuta mtu aliyehusika na shambulio hilo jana kufuatia shambulio  la kigaidi katika kituo  cha  treni  mjini  London. Kitu  ambacho kilifichwa  ndani  ya ndoo  ya  plastiki pamoja  na  mfuko wa kununulia  vitu unaotumika  kwa kuwekwa  katika friji uliripuka ndani ya behewa  la  treni lililojaa  watu , na kuwajeruhi 29, wengi  wao  kwa  kuungua.

England Theresa May verlässt die Downing Street in London
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: REUTERS/T. Melville

"Bila shaka, hiki  kilikuwa  kitu  ambacho  kilikusudiwa kusababisha  madhara  makubwa,"  waziri  mkuu Theresa May  alisema  baada  ya  kuitisha  mkutano  wa  kamati  ya serikali  ya  kuchukua  hatua  za  dharura inayojulikana kama COBRA.

Baadaye jana, May  alisema  kiwango  cha  hatari  kwa nchi  hiyo  kimepandishwa  kutoka  hali  mbaya  na kwenda  juu  zaidi hadi  hali  mbaya  sana, ambayo  ina maana  shambulio  linatarajiwa  wakati  wowote.

"Umma  utashuhudia  polisi  wengi  zaidi  katika  mfumo wa  usafiri  na  katika  mitaa  yetu  wakitoa  ulinzi wa  ziada ," May  amesema.

"Hii  ni  hatua  sahihi  na  inayoeleweka  ambayo  itatoa uhakikisho  wa  ziada  na  ulinzi wakati  mchakato  wa uchunguzi  ukiendelea."

London Explosion in Bahn der Underground
Kamishna msaidizi wa polisi mjini London Mark Rowley akizungumza na waandishi habari kuhusu shambulio mjini humoPicha: picture-alliance/AP Photo/V. Jones

Kundi linalojiita "Dola la Kiislamu"

Kundi linalojiita  Dola  la  Kiislamu  limedai  kundi linalojihusisha  na  kundi  hilo linahusika  na  shambulio hilo, kwa  mujibu wa  kitengo  cha  propaganda  cha  kundi hilo  cha  Amaq. Ofisa  anayehusika  na  kupambana  na ugaidi  nchini  Uingereza  amesema  kundi  la  IS  mara nyingi  hudai  kuhusika  na  mashambulio  ambayo hayajahusika  kabisa  na  kundi  hilo  na  kwamba  maafisa wanatafuta washukiwa  na  vitu  vinavyoweza kusababisha kupatikana kwao.

Watu walioshuhudia  wamesema  kwamba  majeraha yaliyasabishwa  na  mripuko  wenyewe, wakati  kwa wengine yalisababishwa  na  mkanyagano  uliofuatia wakati  abiria  wa  treni  wakijaribu kuharakisha  kutoka  nje ya  kituo  hicho ambacho  kwa  kawaida  kinatumiwa  na watu  wachache.

London Anschlag auf Underground Ubahn
Uchunguzi umeanza kubaini utambulisho wa mshambuliajiPicha: picture-alliance/AP Photo/K. Wigglesworth

Wengine  wanaeleza  kwamba  "mtafaruku ulitokea" wakati mamia  ya  watu  wakijaribu  kukimbia  moto.

"Nilikandamizwa  katika  ngazi. Watu  walikuwa wakiniangukia , watu walizimia, wakilia, kulikuwa  na watoto  wadogo waking'ang'ania  mgongoni  mwangu," Ryan Barnett  mwenye  umri  wa  miaka  25  aliliambia shirika  la  habari  la The Associated Press.

Polisi ya  Uingereza  imesema  mamia  ya  wapepelezi wanafanya  mahojiano ya  dharura  kutaka  kujua utambulisho  wa  mshambuliaji  na  wanasaidiwa  na kitengo  cha  ujasusi.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / ape

Mhariri: Lilian Mtono